ITUTU ATANGAZWA MSHINDI NAFASI YA MWENYEKITI ADC,ASISITIZA UMOJA

 ITUTU ATANGAZWA MSHINDI NAFASI YA MWENYEKITI ADC,ASISITIZA UMOJA




Na Thadei PrayGod, Dar 
Wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama Cha Alliance For Democratic Change (ADC)wamemchagua aliyekuwa Makamo mwenyekiti wa Chama hicho Shaban Itutu kuwa mwenyekiti Mpya wa ADC Taifa akimshinda mpinzani wake Doyo Hassan Doyo.

Mkutano wa chama hicho umefanyika ikiwa ni kukoma Kwa viongozi wa chama hicho ambao wamemaliza muda wao mara baada ya kukitumikia chama Kwa miaka 10 Kwa mujibu wa katiba ya Chama hicho.

Akitangaza matokeo hayo katika uchaguzi huo uliofanyika katika hoteli ya Lamada Jijini Dar Es Salaam jana June 29,2024 Msimamizi wa uchaguzi Mwalimu Aziz alisema Kura halali zilizopigwa na wajumbe zilikuwa 192 ambapo kati ya kura hizo moja iliharibika ambapo katika kura hizo Doyo Hassan Doyo ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho alipata kura 70 huku Shaban Itutu akimshinda Kwa kupata kura 121.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mahindi Itutu alisema kuwa atakiunganisha chama hicho kuwa wamoja baada ya kufanyika Kwa uchaguzi huku akimmwagia sifa Doyo Hassan Doyo Kwa utendaji kazi wake kama Katibu Mkuu.

Itutu aliwaambia wajumbe hao wa mkutano Mkuu ambao walimchagua kuwa atafanya kazi Kwa kushirikiana na Doyo ambaye walikuwa wakishindania nafasi moja kwani ni wanachama wa ADC Kwa miaka mingi hivyo washirikiane kujenga Chama.

Awali akizungumza katika Mkutano huo Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Hamad Rashid aliwashukuru wanachama wa chama hicho Kwa kumpa ushirikiano katika kipindi Chote Cha miaka 10 kama Mwenyekiti wa Taifa wa Chama huku akiwataka kutokiharibu chama hata baada ya kumalizika Kwa uchaguzi.

Mwenyekiti huyo mstaafu aliwaambia wajumbe kwamba Bado ataendelea kusalia kama mwanachama wa Kawaida wa ADC na wakati wowote watakapotaka ushirikiano wake ama ushauri basi wasisite kumtafuta.

Akizungumza Kwenye mkutano huo Mkuu wa nne wa chama hicho ambao pia ulihudhuriwa na Naibu msajili wa vyama vya Siasa Sisty Nyahoza, Mwenyekiti wa Kwanza wa ADC,Said Miraji alisema kwamba uongozi ni karama,Upendo na Unyenyekevu hivyo hakuna budi Kwa watakaoshinda uchaguzi huo kuwa wanyenyekevu na kukiunganisha chama.

"ukiwa kiongozi hupaswi kuwa msema hovyo au mropokaji kwani unakuwa unaongoza chama ambacho ni taasisi na siyo tu utawaongoza unaowaona mbele yako Bali hata watoto wadogo ambao wanategemea malezi ya wazazi/walezi wao hivyo hata baada ya uchaguzi huu muwe wamoja"alisisitiza

Comments