MELI KUBWA YA MATIBABU BURE KUKITA NANGA DAR,JWTZ NA CHINA WAKIFANYA ZOEZI LA PAMOJA LA KIJESHI

 MELI KUBWA YA MATIBABU BURE KUKITA NANGA DAR,JWTZ NA CHINA WAKIFANYA ZOEZI LA PAMOJA LA KIJESHI 



Na Mwandishi wetu, Dar 

SERIKALI ya Tanzania kupitia Jeshi la wananchi wa Tanzania,JWTZ na serikali ya watu wa China kupitia Jeshi la ukombozi wa nchi hiyo wanatarajia kufanya zoezi la pamoja la kijeshi ambalo litaenda sambamba na ujio wa meli kubwa itakayotia nanga katika bandari ya Dar Es Salaam kutoa huduma za Afya Kwa wananchi bila Malipo.


Akizungumza na waandishi wa Habari mapema hii leo Jijini Dar Es Salaam, Kaimu mkurugenzi wa mawasiliano jeshini na msemaji wa JWTZ, Luteni Kanali Gaudence Ilonda amesema zoezi hilo la pamoja kati ya Jeshi la Tanzania na China lijulikanalo kama 'Exercise Amani umoja 2024',litafanyia kuanzia tarehe 29/07/2024 Hadi tarehe 11/08/2024 Katika Mikoa ya Dar Es Salaam na Pwani.


Amesema zoezi la pamoja la kijeshi kati ya Tanzania na China litashirikisha  JWTZ na Jeshi la ukombozi la watu wa China huku JWTZ ikiwa ndiyo mwenyeji wa zoezi hilo.


Ameongeza zoezi hilo litakuwa la wazi na linatarajiwa kufanyika katika sehemu za bahari na nchi kavu likihusisha vifaa na zana mbalimbali za kivita ikiwemo ndege,magari na meli ambapo wananchi watashuhudia zoezi hilo mubashara katika maeneo ambayo litakuwa likifanyika na wengine watashuhudia kupitia Vyombo mbalimbali vya Habari.


"Zoezi pia limelenga kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Jeshi la wananchi wa Tanzania na ushirikiano madhubuti kati ya Jeshi letu na Jeshi la China ambao tumekuwa na ushirikiano nao miaka 60 Sasa Kwa ushirikiano wa kindugu waliyouanzasha Hayati Mwalimu Julius Nyerere na muasisi wa   China"amesema Ilonda.


Kuhusu meli kubwa itakayotia nanga katika bandari ya Dar Es Salaam na kutoa huduma za Afya Kwa wananchi bila Malipo amesema meli hiyo ya matibabu inatarajia kutoa nanga Julai 16,2024 ambapo mbali na wananchi kushuhudia meli hiyo pia watapata fursa ya kuingia ndani yake kupata huduma za kitabibu ambapo pia itakuwa ni Kama sehemu ya utalii wa matibabu  kwa wakazi wa Mkoa wa Dar Es Salaam na maeneo Jirani.


"kupitia mashirikiano yetu kati JWTZ na Jeshi la ukombozi la China sisi kama nchi tutapata fursa ya kujitangaza kijeshi na kiuchumi"ameongeza Msemaji huyo wa jeshi la wananchi wa Tanzania.


Hata hivyo amewataka wananchi wasiwe na wasiwasi na mazoezi hayo ya kijeshi kwani Wana fursa ya kuyatazama katika maeneo ambayo yatakuwa yakifanyika ikiwemo maeneo ya bahari,sambamba na kujitokeza katika zoezi la upimaji wa Afya na matibabu katika meli hiyo kubwa itakayotia nanga bandari ya Dar Es Salaam.

Comments