Skip to main content

WANAOTOA TAARIFA ZA UONGO KUHUSU KUTEKWA KWA WATOTO WAONYWA.

 

WANAOTOA TAARIFA ZA UONGO KUHUSU KUTEKWA KWA WATOTO WAONYWA.


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NA THADEI PRAYGOD

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kupitia Jeshi la Polisi, imesema inafuatilia kwa karibu na itawachukulia hatua wote watakaobainika kujihusisha na tabia ya kutumia vyomvo vya habari na mitandao ya kijamii kuzusha taarifa za uongo zinazohusisha uhalifu ukiwemo wa watoto kupotea au kutekwa na hivyo kuzua taharuki na hofu kubwa kwa jamii ya watanzania. 

Kauli hiyo imetolewa leo Julai 28, 2024 na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo ameeleza kuwa watu hao pia wamekuwa wakitumia taarifa za zamani na kuleta taharuki kwa jamii. 

"Kumeibuka tabia ya baadhi ya watu kutumia vibaya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuzusha taarifa za uongo kwenye jamii zinazohusisha uhalifu ukiwemo wa watoto kupotea au kutekwa na hivyo kuzua taharuki na hofu kubwa kwa jamii ya watanzania. Watu hao wamekuwa wakitumia taarifa za zamani na kuleta taharuki kwa jamii," amesema Mhandisi Masauni na kuongeza. 

"Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kupitia Jeshi la Polisi, inafuatilia kwa karibu na itawachukulia hatua wote watakaobainika kujihusisha na tabia hiyo. Ikumbukwe kuwa kusambaza taarifa za uongo na zisizo na uhakika ni kosa kisheria na ikibainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yako,".

Kwamba ili kudhibiti matukio yote hayo na kuepusha taharuki iliyojitokeza nchini, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi na kwa kushirikiana na Wizara nyingine na Vyombo vingine vya dola imeweka Mkakati madhubuti. 

Mhandisi Masauni ameeleza, mkakati huo unahusisha mambo mablimbali ikiwemo kuongeza elimu kwa umma kuhusu utoaji wa malezi bora na ulinzi kwa watoto. 

"Kwenye hili tutaongeza nguvu zaidi kwa Polisi Kata nchini nzima na pia kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi, Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Elimu Maalum kufikia na kutoa elimi kwa wananchi kwa urahisi," amebainisha Mhandisi Masauni na kuongeza, 

"Tutaimarisha doria za mara kwa mara na kutoa kipaumbele kwenye taarifa wezeshi kutoka kwa wananchi wema. Hii ni pamoja na kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa haraka pale matukio kama hayo yanaporipotiwa Jesho la Polisi. Vilevile, tutaharakisha uchunguzi wa kesi zote za watuhumiwa ambao watabainika kujihusisha na masuala ya uhalifu wa watoto ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukulia haraka,". 

Hata hivyo amebainisha kuwa, hivi karibuni, yamekuwa yakiripotiwa matukio mbalimbali kwenye vyombo vya habari na mengine kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu tuhuma mbalimbali ya vitendo vya kihalifu vinavyohusisha upotevu na utekaji hususan wa watoto wadogo.

Kwamba taarifa zinaonesha baadhi ya watoto hao kufanyiwa vitendo vya kikatili na hata kupelekea kuuawa ambapo matukio hayo yamezua taharuki kubwa kwa wananchi katika baadhi ya Mikoa ikiwemo Dodoma, Dar es  Salaam, Arusha na Kagera.

"Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia uluhu Hassan, kamwe haikubaliani na haitakubaliana na vitendo vyote hivi vya uhalifu wanavyofanyiwa baadhi ya watoto wetu kwani sio tu ni vitendo viovu bali vinaenda kinyume kabisa na utamaduni wa Taifa letu lenye sifa ya Utu, Ustaarabu, Amani na Utulivu. Kwa msingi huo, napenda niwahakikishie ndugu wananchi kuwa Serikali imechukua hatua stahiki wale wote waliobainika na itaendelea kuwachukulia hatua wale watakaobainika kuhusika kwa namna yoyote na matukio haya ya uhalifu," amesema Mhandisi Masauni. 

Ametumia fursa hiyo kuungana na Mheshimiwa Rais na watanzania wote, wakiwemo wa wazazi na walezi, kukemea vikali matukio na aina hii ya uhalifu unaopaswa kukemewa na kila mtanzania na kila mzazi ama mlezi kwani watoto ni Taifa la kesho na wanapaswa kulindwa kwa namna zote na wazazi, walezi na kila mtanzania. 

Hivyo ametoa rai kwa wananchi kushirikiana na Serikali, hususan Jeshi la Polisi, kutoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa washukiwa wote wa matendo haya ya kihalifu. Hii ni pamoja na kuendelea kutoa malezi bora na kuwa karibu na kuwafuatilia watoto wetu wakati wote.

Comments