KAMPUNI YA MWIBA HOLDINGS WAKABIDHI JENGO, BAISKELI 194 KWA WANAFUNZI.

  KAMPUNI YA MWIBA HOLDINGS WAKABIDHI JENGO, BAISKELI 194 KWA WANAFUNZI.



Meneja miradi wa Mwiba Holdings ltd Maetu Sylvester Bwasama akimkabidhi jengo la watumishi wa afya Afisa Tarafa wa Nyalanja Clara Joseph kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Meatu Fauzia Ngatumbura.

Mwandishi Wetu, Meatu

KAMPUNI ya Mwiba Holdings Ltd ambayo imewekeza wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu kufanya shughuli za Utalii na Uhifadhi, juzi imekabidhi jengo la watumishi wa afya na baiskeli 194 kwa wanafunzi vyote vikiwa na thamani ya sh 187.01 milioni.

Jengo lililokabidhiwa litatumiwa na familia tatu za watumishi wa Zahanati ya Kijiji cha Mwamhongo , wakati Baiskeli 194 zitatumiwa na wanafunzi wanaosema shule ya Busangwa ambao wanatoka vijiji vya Ming’ongwa, Butuli, Bulyandulu na Sakasaka.

Akizungumza wakati wa kukabidhi, jengo la watumishi wa afya na Baiskeli hizo,meneja miradi ya Maendeleo ya jamii ya Mwiba Holdings Ltd wilayani Meatu,Sylvester Bwasama alisema lengo la miradi hiyo ni kusaidia watumishi wa afya kutoa huduma bora na wanafunzi kufika shuleni kwa wakati na hivyo kuongeza ufaulu.

Bwasama alisema Mwiba Holdings Limited ni miongoni mwa makampuni dada ya Friedkin Tanzania Companies ambayo yanajihusisha na shughuli za uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori na utalii katika wilaya hiyo tangu mwaka 2008.

Alisema Kampuni ya Mwiba Holdings Ltd imewekeza katika wilaya ya Meatu katika mapori ya hifadhi ya Kijiji cha Makao na Pori la Akiba Maswa na miradi hiyo ni sehemu tu ya miradi ya jamii ambayo inatekelezwa wilayani Meatu.

“leo tunafaraja kubwa hapa kukabidhi Nyumba ya watumishi wa zahanati ya kijiji cha Mwamhongo yenye uwezo wa kuhudumia familia tatu kuishi kwa Pamoja na Lengo la mradi huu ni kuwezesha watumishi wa afya watakao letwa hapa kuhudumia wanachi wa Mwamhongo kuishi katika makazi bora yanayovutia watumishi kuendelea kuwepo maeneo haya.

Alisema mradi huo,umegharimu kiasi cha Tsh 130,369,452 milioni ambapo na Mkandarasi alikuwa ni Damaki Investment Company ambayo ni kampuni ya wilayani Meatu.

Akizungumza wakati wa kukabidhi baiskeli 194 kwa wanafunzi wanaoishi mbali na shule ya Busangwa, alisema zitasaidia wanafunzi wanaotoka vijiji vya Ming’ongwa, Butuli, Bulyandulu na Sakasaka kufika shuleni kwa wakati na usalama.

“lengo la kutolewa baiskeli hizi ni kuwezesha wanafunzi kuwahi shuleni waweze kuwa na muda mwingi wa kujifunza na kuwahi kurudi majumbani kwao na zimegharimu kiasi cha Tsh 56,650,000 milioniälisema

“Wazo la kuanzisha mradi huu lilitokana na ukweli kwamba wanafunzi wamekuwa wakitembea kutoka vijiiji husika na kufika shuleni kwa miguu na Tulifanya tathimini ya kutafuta aina gani ya usafiri unaoweza kuwafikia wanafunzi wengi na isiyokuwa na changamoto nyingi, Baiskeli zilionekana kuwa aina bora ya usafiri ambayo ni rahisi kutumiwa na wanafunzi”alisema

 

Alisema Mradi huu utakuwa endelevu kwani, pale ambapo mwanafunzi atahitimu masomo atapaswa kuikabidhi baiskeli kwenye uongozi wa shule ili atakayejiunga na shule aweze kuitumia kwa muda atakapokuwa hapa shuleni.

 

“ Ili kufanikisha hilo, tumeweka utaratibu wa ufuatiliaji na usimamizi kwa kushirikiana na walimu na kuhakikisha baiskeli hizo zinafanyiwa ukarabati na kampuni ya Mwiba Holdings Ltd pale inapohitajika”alisema

Alisema Mwiba Hodings Ltd kupitia Friedkin Conservation Fund itaendelea kutekeleza miradi ya jamii kwa kadri ya upatikanaji wa fedha na kwa kuzingatia makubaliano waliyonayo chini ya Mkataba wa SWICA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori (TAWA) na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu.

Alisema Mradi huo ni miongoni mwa miradi na shughuli tulizoahidi kuzifanya kwa mwaka 2023 kwenye kikao cha wadau. Miradi mingine iliyokamilika hivi karibuni ni nyumba ya walimu na madarasa mawili katika shule ya msingi Mwajimoso iliyopo kijiji cha Mwabagimu

Miradi mingine ni Ujenzi wa nyumba ya wahudumu wa afya katika zahanati mpya ya kijiji cha Mwamhongo, kufadhili chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule ya msingi Makao,Kufadhili matibabu ya watoto walemavu wa viungo na Kufadhili masomo ya wanafunzi wanaofanya vizuri na wenye uhitaji ngazi za sekondari na vyuo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Meatu,, Fauzia Ngatumbura, Afisa Tarafa ya Nyalanja Clara Joseph alipongeza kampuni ya Mwiba Holdings Ltd na Friedkin kwa misaada ambayo wameendelea kutoa katika wilaya hiyo.

Joseph aliagiza watumishi wa afya ambao watakaa katika jengo hilo, kutunza na kutoa huduma bora kwa wananchi lakini, pia aliwataka wanafunzi ambao watakabidhiwa Baiskeli hizo wazitunze ili zitumike kwa muda mrefu na wanafunzi wengine.

Jeremia Masunga mkazi wa Kijiji cha Butuli, apongeza kampuni ya Mwiba kuendelea kusaidia miradi ya jamii na kueleza wananchi wa Meatu wataendelea kuiunga mkono kampuni hiyo, kwani imekuwa na manufaa makubwa kwao

Comments