RAIS DKT. SAMIA KUSHIRIKI MKUTANO WA USHIRIKIANO WA CHINA NA AFRIKA( FOCAC) NCHINI CHINA

 RAIS DKT. SAMIA KUSHIRIKI MKUTANO WA FOCAC NCHINI CHINA


Na Thadei PrayGod

Rais wa Jamhuri wa Muungano Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika(FOCAC) utakaofanyika kuanzia Septemba 4 hadi 6  2024 jijini Beijing, China.

Taarifa hiyo imetolewa leo Agost 31,2024 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo (MB) wakati akizungumza na Waandishi wa habari nakubainisha kuwa Dkt Samia anashiriki Mkutano huo kufuatia mwaliko wa  Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Xi Jinping.

Aidha Balozi Kombo amesema kuwa, ushiriki wa Rais  DKT Samia kwenye Mkutano huo  wa kilele wa FOCAC umelenga kuendelea kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China ambao mwaka huu umetimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Nchi hizo mbili.

Amesema kuwa Mkutano huo utawezesha kujadiliana na kukubaliana na China  namna ya kuendelea kuongeza ushirikiano katika maeneo ya kipaumbele kwa maendeleo  ya Taifa ikiwemo katika sekta ya miundombinu, mifumo ya chakula, biashara na uwekezaji, kubadilishana ujuzi, upatikanaji wa nishati safi na salama na kusaidia ujenzi wa uchumi wa kidijitali. 

Ameongeza kuwa,utasaidia kuibua fursa mpya za ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili pamoja na kutangaza maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya Sita ya sera na sheria katika sekta ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka nchini humo.

Aidha, Serikali ya China imemteua Rais Dkt. Samia kuhutubia kwenye hafla ya ufunguzi wa mkutano huo wa Kilele wa wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC akiwakilisha Kanda ya Afrika Mashariki, huku kauli mbiu ikiwa “Kushirikiana ili Kuendeleza Usasa na Kujenga Jamii Bora ya China na Afrika kwa Mustakabali wa Pamoja"

Amesema kuwa, ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo utaongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ataungana na wakuu wa Nchi na Serikali wenzake kutoka Nchi zaidi ya 40 kati ya 54 za Bara la Afrika kushiriki Mkutano huo.

Balozi Kombo amefafanua kuwa Jukwaa la FOCAC lilianzishwa mwaka 2000 na Jamhuri ya watu wa China kwa lengo la kukuza ushirikiano na maendeleo ya pamoja kati ya China na Afrika,  ambapo tangu kuanzishwa kwake jumla ya mikutano ya Kilele (Wakuu wa Nchi na Serikali) nane (8) imefanyika.

"Mikutano hiyo hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa kubalishana kati ya China na nchi moja ya Afrika, mkutano huu wa 9 wa FOCAC utafungulia na Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China ambapo, hotuba yake ya ufunguzi itatoa uelekeo wa China katika uhusiano wake na nchi za Afrika, 

Aidha, viongozi mbalimbali watashiriki katika mkutano huo ikiwa ni pamoja na Antonia Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Moussa Faki, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika watashiriki Mkutano huo.

Amesema kuwa mada zitakazojadiliwa ni pamoja na Utawala wa Nchi, Mpango wa Miundombinu na Uwekezaji, Maendeleo ya Viwanda na Kilimo cha Kisasa na Amani na Usalama, kwa upande wa Tanzania utajikita kwenye mada ya Maendeleo ya Viwanda na Kilimo cha Kisasa mada hiyo imezingatia Mpango wa Maendeleo wa Tatu wa Miaka Mitano, ambao ndiyo mpango wa mwisho wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025.

Amesema Tanzania inatarajia kuwasilisha miradi mbalimbali ikiwemo mipya na ile ambayo haiweza kutelezwa kwenye mpango uliopita wa FOCAC kwa sababu mbalimbali, ili iweze kutekelezwa chini ya mpango kazi wa FOCAC kwa kipindi cha 2025-2027 kwa kupatiwa fedha za mkopo nafuu na msaada.

Miradi hiyo ni pamoja na Ujenzi wa Mtandao wa Mawasiliano Vijijini wa awamu ya pili, Ujenzi wa njia ya kusafirisha Umeme wa Kv 400 wa awamu ya Pili na Tatu , Ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) wa awamu ya Pili na Ujenzi wa Babara za Zanzibar Zenye Urefu wa Kilomita 277.7 .

Comments