Skip to main content

WMA YAHAMASISHA MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO KWA WATUMISHI NSSF ILALA




Na Mahamudu Jamal - WMA

Wakala wa Vipimo  Tanzania (WMA), imewahamasisha watumishi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Ilala, kujenga tabia ya kuwa makini  na  namna vipimo vinavyotumika kila wanapopata huduma na mahitaji mbalimbali.

Afisa Vipimo kutoka WMA Ilala, Yahaya Tunda, amesisitiza hay oleo, Agosti 28, 2024 wakati akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya WMA kwa watumishi hao wa NSSF, ambapo amebainisha kuwa jukumu kubwa la Wakala ni kumlinda mwananchi dhidi ya matumizi batili ya vipimo katika maeneo ya biashara, afya, usalama na mazingira.

Aidha, ameongeza kuwa majukumu mengine ya WMA ni kuiwakilisha nchi katika masuala ya Kivipimo ya kikanda na dunia, kufanya ukaguzi katika maeneo ya uzalishaji, njia za usafiri na maeneo ya biashara, na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa taasisi na wadau wa vipimo.

Tunda amefafanua kuwa, pamoja na kwamba WMA inawajibika kumlinda mwananchi dhidi ya matumizi batili ya vipimo, lakini wananchi pia wanapaswa kujilinda na kuchukua tahadhari hususani wanapopata huduma au mahitaji.

“Ni vyema kuwa makini na kujiridhisha kwamba vipimo vinavyotumiwa na mfanyabiashara ni sahihi na vimehakikiwa na WMA. Mathalani, ukienda kununua mbao, nenda na futi yako iliyohakikiwa, halikadhalika ukienda kununua saruji hakikisha inapimwa kwa usahihi kwenye mizani iliyohakikiwa. Vivyo hivyo kwa nyama, mboga mboga na bidhaa nyingine zote.”

Akifafanua zaidi, amesema kwa wenye magari, wanapokuwa katika vituo vya kujazia mafuta,  wahakikishe wanakuwa makini pindi wanapohudumiwa, na ikitokea kutoridhishwa na upimaji husika, wawasilishe shauri hilo katika Ofisi za WMA zilizoko mikoa yote Tanzania Bara pamoja na mipaka yote ya nchi ili kusaidia kupunguza athari za udanganyifu katika vipimo na hivyo kuchagiza maendeleo.

Vilevile, ameongeza kuwa WMA inaendelea kupanua wigo wa huduma zake kwa kujikita katika maeneo mapya ya uhakiki wa Dira za Maji na Mita za Umeme ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na usawa katika utoaji wa huduma na malipo sahihi ya huduma hizo.

“Tunahakiki Dira zote za Maji na Mita za Umeme, lakini pia kupitia Kitengo chetu cha Bandari tunahakiki mafuta yote yanayoingia nchini na yale yanayosafirishwa kwenda nchi jirani,” amesema Tunda.

Kwa upande wake, Afisa Tawala Mwandamizi NSSF Ilala, Sarah Mashalla, ameishukuru WMA kuona umuhimu wa kutoa elimu ya vipimo kwa watumishi hao katika zoezi endelevu linalolenga kuyafikia makundi mbalimbali ya jamii.

“WMA wametufumbua macho kuhusu vipimo kupitia semina hii. Nasi sasa tutaongeza umakini wakati tukifanya manunuzi ya bidhaa pamoja na huduma mbalimbali. Tunaahidi kuwa mabalozi wazuri kwa watumishi wengine na hata jamii kwa ujumla. Tunataka tuione Tanzania yenye haki na maendeleo katika kila sehemu,” amesema.

WMA inaendelea na Kampeni ya kutoa elimu ya vipimo kwa umma kupitia makundi mbalimbali ili kuwajengea uelewa wa vipimo sahihi pamoja na manufaa yake kwa wafanyabiashara na walaji.

Comments