HESLB Yaanza kutangaza orodha ya wanafunzi watakaopata mikopo Kwa mwaka wa masomo 2024/2025,ni 21,509 yasema waombaji wote waliokidhi vigezo watapata.

 HESLB Yaanza kutangaza orodha ya wanafunzi watakaopata mikopo Kwa mwaka wa masomo 2024/2025,ni 21,509 yasema waombaji wote waliokidhi vigezo watapata.




NA THADEI PRAYGOD 

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu hapa nchini (HESLB)Leo imetangaza orodha ya  awamu ya kwanza ya wanafunzi wanufaika waliopangiwa kupata mikopo kwa mwaka wa masomo 2024/2025.

Akizungumza na waandishi wa Habari Leo Septemba 28,2024 Jijini Dar Es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo Dkt Bill Kiwia amesema orodha hiyo ya awamu ya kwanza inajumuisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo ya shahada ya awali,Shule ya Sheria Kwa vitendo na shahada ya uzamili.

Amesema orodha hiyo ya awamu ya kwanza wanafunzi 21,509 wataanza kupatiwa mikopo ambapo jumla ya shilingi za kitanzania bilioni 70.78 zinatumika.

"Leo tumeanza kutoa taarifa za mikopo kwa makundi yote,waliopangiwa mikopo,wapo ambao bado tunaendelea kufanyia kazi maombi yao na kila mwombaji atapata taarifa yake kwenye akaunti yake ile ile aloyotumia kuombea mikopo,na Wala hauhitaji kufika ofisi za HESLB"amesema Dkt Kiwia huku akisisitiza kuwa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada na shahada ya uzamivu unaendelea.


Aidha Dkt Kiwia amesema kuwa bodi hiyo imeanza kuandaa malipo ya wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo ambao ni wanufaika wa mikopo,lengo likiwa ni kuhakikisha fedha zinafika vyuoni Kwa wakati huku akivitaka vyuo kuwasilisha matokeo ya mitihani ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo wanaoendelea na masomo ili malipo yao yaandaliwe Kwa wakati bila kicheleweshwa.

"Kuna vyuo vichache,ambavyo bado havijawasilisha matokeo,tumewakumbusha na kuwasisitiza waharakishe kuwasilisha matokeo ya mitihani ya wanufaika ili na sisi tukamilishe malipo ya wanafunzi waliofaulu kuendelea na masomo"amesema Dkt Kiwia.

Amesema wanafunzi waliopangiwa kupata mikopo watapata taarifa kupitia simu zao za mikononi 'simu janja' au kompyuta kupitia akaunti zao walizoombea mikopo zijulikanazo kama 'SIPA'- Student's Individual Permanent Account.

Kuhusu mikopo hiyo Dkt Kiwia amesema kuwa Kwa mwaka huu,serikali imetenga Shilingi bilioni 787 Kwa ajili ya jumla ya wanafunzi 245,799 wakiwemo zaidi ya wanafunzi 88,000 wa mwaka wa kwanza waliotengewa bilioni 284.8 na kuongeza kuwa bajeti hiyo ya mwaka 2024/2025 imeongezeka Kwa shilingi bilioni 38 sawa na asilimia 5 ikilinganishwa na bajeti ya 2023/2024 ambayo ilikuwa ni bilioni 749.

Hata hivyo Dkt Kiwia amesema kuwa kupitia elimu waliyoitoa katika Shule za Msingi na sekondari Mikoa yote 31 kuhusu namna ya kuomba mikopo imesaidia kupunguza makosa Kwa waombaji kwani hapo awali kulikuwa na changamoto kubwa Kwa waombaji kukosea kuomba Jambo lililochelewesha mchakato na kuongeza kuwa Kwa mwaka wa masomo 2024/2025 wanufaika wa Mikopo pia watanufaika na ongezeko la mikopo hasa katika ada vyuoni.

Kwa upande wake rais wa jumuiya ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu na vya Kati,TAHLISO Bi Zainab Kitima ameishukuru serikali chini ya usimamizi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutoka shilingi 200,000 hadi 530,000 kwa kusema kuwa Sasa ongezeko hilo litapunguza mzigo Kwa wazazi na wanafunzi hasa wanaotokea kwenye familia zenye hali duni.

"Tunaishukuru sana serikali Leo kupitia HESLB tumesikia Mkurugenzi Dkt Kiwia akisema kuwa mikopo itafikishwa vyuoni Kwa wakati,ni taarifa njema sana Kwa wanufaika wa Mikopo ya elimu ya juu kote nchini"amesema.

Orodha ya awamu ya pili ya wanafunzi waliopangiwa mikopo Kwa mwaka wa masomo 2024/2025 inatarajiwa kutangazwa wiki ijayo na bodi hiyo ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (HESLB).

Comments