Skip to main content

RAIS SAMIA ASEMA AJENDA YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA INALENGA ZAIDI WANAWAKE AFRIKA

 

RAIS SAMIA ASEMA AJENDA YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA INALENGA ZAIDI WANAWAKE AFRIKA



Na Mwandishi Wetu 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.  Samia Suluhu Hassan amesema sasa ni wakati wa Bara la Afrika kubadilika kwa kutumia Nishati Safi ya Kupikia ili kutoathiri afya na mazingira kutokana na matumizi ya nishati zisizo safi kama kuni na mkaa.

Dkt. Samia ameyasema hayo leo Septemba 27, 2024 wakati akizindua Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Iliyopo Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ambayo imefungiwa mifumo ya Nishati Safi ya Kupikia.

"Kilichonifurahisha zaidi nilipofika hapa ni matumizi ya nishati safi ya kupikia, huu ni mradi wangu nilioubeba kwa ajili ya wanawake wa Afrika." Amesema Rais Samia

Ameongeza kuwa, Wanawake wengi Afrika wamekuwa wakipata maradhi kwa ajili ya matumizi ya nishati zisizo safi kama kuni na hivyo kupoteza maisha.

Amesisitiza kuwa, hivi sasa Taasisi kubwa ikiwemo za elimu ambazo zina idadi ya zaidi ya watu mia moja Serikali itaanza nazo kwa kuzifungia mifumo ya  nishati safi ya kupikia.

Awali, Naibu Waziri Nishati,  Mhe. Judith Kapinga amesema mradi huo wa nishati safi katika shule hiyo umetekelezwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) huku Oryx Gas wakifadhili mtungi mkubwa wa kilo 1,750.

"Hapa watakuwa na uwezo wa kutumia nishati hii kwa mwezi mmoja na nusu hadi miezi miwili, hivi sasa wana wanafunzi takriban 500 lakini majiko haya yanauwezo wa kupikia hadi wanafunzi 800."  Amefafanua Kapinga 

Ameongeza kuwa, pamoja na kufungwa kwa mifumo hiyo, elimu  ya matumizi sahihi ya nishati safi ya kupikia imetolewa shuleni hapo.

Comments