Tusifanye siasa za hovyo Kwa kutukana na kudhalilisha viongozi:DOYO
Tusifanye siasa za hovyo,kutukana na kudhalilisha viongozi:DOYO
NA MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu wa chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo amewataka wanasiasa nchini kuacha kiburi na kutowaheshimu viongozi walio madarakani Kwa kufanya siasa ambazo zinadhalilisha na kuchafua watu Kwa kutweza utu wao.
Doyo ameyasema hayo Leo Septemba 29,2024 katika Uzinduzi wa program ya chama hicho kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 uliofanyika katika ofisi za Makao makuu ya chama hicho zilizopo Tandika,Temeke Jijini Dar Es Salaam
"Juzi Kuna Kongamano la chama fulani la wanawake lilikuwa likimtuhumu Rais kuwa ni muuaji hiyo siyo sawa kwani kama Mungu amekupangia Kifo utakufa tuu"amesema
Ameongeza kuwa chama hicho kimesikitishwa na tuhuma za chama hicho na kuviomba vyombo vya usalama kuchukua hatua stahiki kwa wanaomchafua Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Aidha ameongeza kuwa chama hicho kitafanya siasa safi na kutoa wito kwa wanachama wake kutotoa maneno ya kashfa na kutweza utu wa mtu na waheshimu Mamlaka kwa kuwa na Uhuru wenye mipaka.
"Katika itikadi ya chama chetu tunaamini kuwepo Kwa Uhuru ila wenye mipaka na wa kujenga hoja juu ya namna gani wanaweza kuwasaidia watanzania kutatua changamoto zao na si kutukana diwani,mbunge au Rais wa nchi hivyo nawasihi wanachama wa NLD mkaawaambie watanzania namna mtakavyowakwamua na kujenga hoja za maendeleo,mtapata wanachama bila kutukana viongozi kwani nao wana watoto"amesema.
Kuhusu chama hicho Doyo amesema kuwa wamezindua mpango mkakati ambao umekuja na Oparesheni fyeka CCM Kwa kutengeneza wagombea watakaoleta ushindani katika uchaguzi wa serikali za mitaa na kushinda Kwa kishindo uchaguzi huo.
Aidha amelalamikia kalenda (ratiba)ya uchaguzi wa serikali za mitaa ambayo imebana na haitoi muda wa kutosha Kwa vyama kujiandaa na kujipanga vyema.
"Tamisemi isipime vyama vyetu kwamba vinaweza kushindana na chama tawala Kwa kufanya kampeni muda siku Saba pekee,hivyo tunaomba ratiba iongezwe muda ili tuweze kumudu hali ya uchaguzi kwani Kwa namna vyama vyetu hali zake zilivyo inaleta shida na hatusemi uchaguzi uhairishwe huo siyo msimamo wetu tunaomba tu ziongezwe siku ili tujipange vyema",amesema.
Amesema chama hicho kitasimamisha wagombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na tayari timu yake iko Mikoani kuhakikisha wagombea wanapatikana.
Naye katibu Mkuu mstaafu wa NLD Tozy Matwanga amesema kuwa ili kujenga serikali ni lazima chama kiingie katika uchaguzi,hivyo na wao Kama chama watashiriki chaguzi zote na hawatogomea.
Hata hivyo chama hicho kimewapokea wanachama wapya kutoka chama cha ACT Wazalendo na ADC akiwemo Bi Mariam Ahmed Sijaona ambaye alikuwa mjumbe wa halmashauri kuu ngome ya wanawake Taifa ya ACT ambaye amesema amechukua maamuzi ya kukikacha na kujiunga na NLD baada ya kusoma na kuridhishwa na Sera zake.
Comments