NBS YASEMA TAARIFA ILIYOTOLEWA NA SERIKALI JUU YA IDADI YA WALIOJIANDIKISHA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA NI SAHIHI,yakemea upotoshaji

 



NA MWANDISHI WETU 

OFISI ya Taifa  ya Takwimu(NBS)  imesema taarifa iliyotolewa na serikali ya idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu, ni sahihi na ni takwimu za serikali.

Kauli hiyo imekuja ikiwa zimepita siku chache, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa kutoa taarifa juu ya matokeo ya zoezi la uandikishaji wapiga kura wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika  Novemba 27, mwaka huu.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa wakati akitoa ufafanuzi wa takwimu  za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 zilizotumika  katika uandikishaji wa orofha ya wapigakura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mapema mwaka huu.

“Taarifa hiyo ya Serikali ilionesha kuwa, wananchi waliojiandikisha kushiriki katika uchaguzi huo ni 31,282,331 sawa na asilimia 94.83 ya watu wote wenye umri wa kujiandikisha kwa mwaka 2024.

“Hata hivyo, tangu kutolewa kwa taarifa hiyo, kumekuwepo na taarifa za kupotosha takwimu hizo kwenye baadhi ya vyombo vya habari hususan mitandao ya kijamii kwamba takwimu za wananchi walioandikishwa hazina uhalisia na kwamba idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na idadi ya watu wanaostahili kujiandikisha kupiga kura inayotokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022,” alisema.

Dk. Albina alisema takwimu wanazozizungumzia watu hao ni takwimu zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 na kwamba ulinganishaji wanaoufanya hauendani na hali halisi ya idadi ya watu wenye sifa za kujiandikisha kupiga kura mwaka huu.

Alisema  kwa hesabu za kawaida idadi ya watu nchini kwa mwaka 2022 haiwezi kulingana na idadi ya watu kwa mwaka 2024 kwani hivi sasa tayari miaka miwili kamili imeshapita tangu ikufanyika kwa sensa hiyo.

 “Kutokana na makadirio ya idadi ya watu kwa 2024, idadi ya watu nchini inakadiriwa kuwa Milioni 66.3 sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 3.2 kwa mwaka kama ilivyopatikana kwenye Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

“Makadirio haya kwa Tanzania Bara yanakadiriwa kufikia watu milioni 64.2 na kwa Tanzania Zanzibar yanakadiriwa kufikia watu milioni 2.03, kwa makadirio haya, wananchi tunapaswa kufahamu kuwa idadi ya watu kwa mwaka 2024 haiwezi kuwa sawasawa na ile ya mwaka 2022,” alisema.

Alifafanua kuwa watu waliokuwa na umri wa miaka 16, 17 na 18 katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 hivi sasa wana umri wa miaka 18, 19 na 20 ambao idadi yao ni 3,785,036 waliokidhi kigezo cha umri wa kujiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mwaka huu.

Alisema idadi ya watu wenye umri wa kupiga kura ni sawa na watu wote ambao mwaka 2022 walikuwa na umri wa miaka 16 na zaidi ama kwa lugha nyingine ni wote ambao ifikapo Novemba  27, mwaka huu, watakuwa wametimiza umri wa miaka 18 au zaidi.

“Kwa mahesabu hayo yanayotokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, makadirio ya idadi hiyo ya watu wenye umri wa kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambayo ni watu 32,987,579 ni sahihi na ni rasmi kulingana na Kanunuzi za Msingi za Umoja wa Mataifa Kuhusu Takwimu Rasmi na kama ilivyoripotiwa kwenye taarifa ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI,” alisema.

UANDIKISHAJI KWA MIKOA

Dk. Albina alisema kuhusu kiwango cha uandikishaji kwa mikoa, imejitokeza baadhi yake kuwa na asilimia zaidi ya 100 ya watu walioandikishwa  na kufafanua kuwa watu wana tabia ya kuhamahama kutoka eneo moja kwenda eneo na kusababisha uandikishaji wa watu wengi zaidi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa baadhi ya mikoa.

“Itakumbukwa kuwa, Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ilihesabu watu kulingana na mahali walipolala usiku wa kuamkia siku ya Sensa yaani Agosti 23, 2022. Kwa hivyo, hili ni jambo la kawaida na linalowezekana kutokea kama ilivyotokea katika mikoa hiyo ya Pwani (asilimia 112.61); Tanga (asilimia 110.82); Mwanza (asilimia 106.58); Dodoma (asilmia 104.19) na Iringa (asilimia 100.54),” alisema.

 Alisema idadi kubwa ya watu mkoa wa Pwani inatokana na watu wengi wa Dar es Salaam kuwa na makazi mkoa wa Pwani hasa katika wilaya za Bagamoyo, Kibaha, Kisarawe na Mkuranga. Kwa hiyo ongezeko hilo la watu kwenye maeneo hayo linachangiwa na kuhama kwa watu na si kwa kuandikisha watu waliokosa sifa.

Mikoa yenye asilimia ndogo ya uandikishaji ni ile ambayo chambuzi za kitakwimu zinaonesha ni mikoa yenye uhamaji mkubwa wa watu kwenda katika majiji.

TAKWIMU ZA SENSA KWA MAKUNDI

Dk. Albina alitoa takwimu za sensa kwa makundi ya umri  na kusema kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, idadi ya watoto walio na umri chini ya miaka 15 nchini ilikuwa 26,399,989 sawa na asilimia 42.8.

Pia idadi ya watu wenye umri wa kufanya kazi wenye umri miaka 15 hadi 64 walikuwa 33,000,128 sawa na asilimia 53.4 na idadi ya wazee walikuwa 2,341,003 sawa na asilimia 3.8.

Alifafanua kuwa wastani wa watoto chini ya umri wa miaka 15 kuwa ni asilimia 60 hadi 70 ni upotoshaji mkubwa kwani hata viwango vya Afrika, asilimia ya watoto ni kati ya asilimia 40 hadi 45 na si vinginevyo.

“Hizi ndizo takwimu rasmi za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu sura 351 kwa maana hiyo, taarifa iliyotolewa na Serikali ya Idadi ya wananchi waliojiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba, 2024 ni sahihi kwa sababu kiujumla idadi ya watu wote waliojiandikisha nchini haijavuka ile inayotokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022,” alisema

Alisema takwimu hizo hazina mashaka yoyote na kuonya kutopotosha umma  kwani ni kosa kisheria kupotosha umma kwa kutumia takwimu rasmi kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu.

Kwa upande wake, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Bara, Spika Mstaafu Anne Makinda aliwataka Watanzania kuacha upotoshaji kwani takwimu zilizopo ni sahihi na zimefuata vigezo vyote.

“Hii ndio taarifa rasmi, takwimu za sensa ndio msingi wa kufanyia kitu kama  zisingekuwepo  tusingepata asilimia, takwimu za sensa ni mwongozo wa kufanya mambo yote ya maendeleo,” alisema.


=======

Comments