TMA YATOA TAHADHARI KWA WAKULIMA,YAWATAKA KUZINGATIA TAARIFA ZA UTABIRI WAKE,yatangaza utabiri wa msimu wa mvua Novemba 2024 Hadi April 2025

 


NA MWANDISHI WETU 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imehimiza wakulima kote nchini kuchukua hatua makini kwa kuzingatia utabiri wa hali ya hewa unaotolewa kwa kila wilaya ili kufanikisha uchaguzi bora wa mbegu na mazao. Ushauri huu unalenga kuwasaidia wakulima kuendana na hali halisi ya msimu na kuepuka hasara zisizo za lazima.

Akizungumza leo Oktoba 31, 2024, jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), amesema kuwa mvua za msimu wa Novemba 2024 hadi Aprili 2025 zinatarajiwa kuleta mafanikio kwa baadhi ya maeneo, huku nyanda za juu kaskazini mashariki zikikumbwa na ukavu unaoendelea.

"Mvua hizi zimeanza kuonekana katika maeneo ya Ziwa Victoria na pwani ya kaskazini," alisema Dkt. Chang'a, akiongeza kuwa mwelekeo wa mvua za msimu unatarajiwa kuleta athari tofauti kulingana na eneo husika. Maeneo ya magharibi, kanda ya kati, nyanda za juu kusini magharibi, na kusini mwa Tanzania yanatarajia mvua, huku viwango vya mvua vikitarajiwa kuwa wastani hadi chini ya wastani kwa mikoa kama Kigoma, Tabora, na Dodoma. Aidha, mikoa ya Njombe, Ruvuma, na Mtwara inatarajia mvua za wastani hadi juu ya wastani, haswa kati ya Februari na Aprili 2025.

Kwa upande wa sekta za mifugo na uvuvi, Dkt. Chang'a amesema kuwa mvua hizi zinatarajiwa kuongeza upatikanaji wa malisho na maji, hali ambayo inatarajiwa kuleta mafanikio kwa wafugaji na wavuvi. Hata hivyo, aliwaonya wafugaji kuhusu hatari ya magonjwa kama homa ya bonde la ufa na wadudu wadhurifu wanaoweza kujitokeza.

Alisema, "Ni muhimu wafugaji kupanga matumizi bora ya maji na malisho, pamoja na kufuata ushauri wa maofisa ugani ili kukabiliana na changamoto zinazoweza kuibuka na kunufaika na hali ya hewa inayotarajiwa."

Kwa ujumla, Dkt. Chang'a amewahimiza wakulima, wafugaji, na wavuvi kutumia taarifa za utabiri wa hali ya hewa kwa ukaribu ili kufanikisha mipango ya msimu huu na kujiepusha na changamoto zinazoweza kujitokeza.

Comments