TUNAIMARISHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI NA MIUNDOMBINU YA NISHATI ILI KUFIKISHA HUDUMA KWA WOTE- DKT.MATARAGIO
TUNAIMARISHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI NA MIUNDOMBINU YA NISHATI ILI KUFIKISHA HUDUMA KWA WOTE- DKT.MATARAGIO
📌 Asisitiza nia ya Serikali ni kutoa huduma stahiki bila kuangalia umbali au kipato
📌 Apongeza kampuni ya Puma Energy Tanzania kushirikiana na Serikali uhamasishaji Nishati Safi ya Kupikia
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amesema Serikali inaendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji na miundombinu ya Sekta ya Nishati nchini ili kuwezesha wananchi kufikiwa na huduma stahiki bila kujali umbali na vipato vyao.
Dkt. Mataragio ameyaeleza hayo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utoaji Tuzo kwa Mawakala na Wadau wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania ambayo inaunga mkono juhudi za Serikali za kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia bidhaa za Puma Gas.
Dkt. Mataragio amesema moja ya majukumu ya Wizara ya Nishati ni kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo watoa huduma na watumiaji ili kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali utakaopelekea utoaji wa huduma bora kwa wananchi ikiwa ni moja ya vipaumbele vya Serikali.
Katika hafla hiyo, Dkt.Mataragio ameipongeza kampuni ya Puma kwa jitihada zinazounga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuhamasisha jamii ili itumie Nishati Safi ya Kupikia na hivyo kutimiza lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo mwaka 2034.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa Balozi na kinara katika kuhamasisha matumizi ya Nshati Safi ya Kupikia nchini na Duniani ili kuhakikisha Watu wanaondokana na matumizi ya kuni na mkaa ambao una madhara kwa afya na kusababisha uharibifu wa mazingira.
Kuhusu Tuzo hizo zilizotolewa na Puma Energy Tanzania kwa Mawakala na Wadau mbalimbali nchini, Dkt.Mataragio ameelekeza kuwa ziwe chachu ya kuendelea kufanya kazi kwa weledi na ufanisi kulingana na vigezo na mashariti ya Kampuni kwa maslahi ya jamii.
Amesema kupitia mfano uliooneshwa na Puma Energy Tanzania wa kuwakutanisha wadau wake kila mwaka ili kuzungumzia mafanikio na changamoto zilizopatikana, iwe ni chachu kwa kampuni nyingine kuiga mfano huo ambao unasaidia kukuza sekta ya Nishati nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania, Bi. Fatuma Abdallah ameishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali za kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kuwafikishia wananchi bidhaa ya Puma Gas kupitia kwa Mawakala na Wadau waliopo maeneo mbalimbali.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Kamishna wa Petroli na Gesi, Godluck Shirima.
Comments