WAANDISHI BORA WA HABARI ZA HALI YA HEWA WATUNIKIWA TUZO

 WAANDISHI BORA WA HABARI ZA HALI YA HEWA WATUNIKIWA TUZO



Dar es Salaam, Tarehe 28 Oktoba 2024.

Mwenyekiti wa Bodi Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari amewatunukia rasmi tuzo waandishi wa habari waliofanya vizuri kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2023 hadi Juni 2024 katika kuandika habari za hali ya hewa nchini. Hafla hiyo fupi ilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Dar es Salaam, tarehe 28 Oktoba 2024.


Kabla ya kukadidhi tuzo hizo kwa washindi, Mhe. Mshibe ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo aliipongeza TMA kwa kuendelea kuwashirikisha na kutoa motisha kwa wanahabari katika utoaji elimu na usambazaji wa huduma za hali ya hewa 

Alieleza kuwa, TMA ni moja ya taasis chache nchini, zinazothamini mchango wa wanahabari kwa ujumla ikiwemo ubunifu wa kuanzisha TUZO ya wanahabari bora wa habari za hali ya hewa nchini kwa miaka mitano sasa, ambapo kwa mwaka huu nimeelezwa kuwa TMA imeongeza wigo wa washindi.

“Katika kuhakikisha tuzo hizi zinaendelea kuwa bora zaidi, mwaka huu Mamlaka imeboresha maeneo kadhaa ikiwemo kuongeza vipengele viwili vya waandishi kutoka nje ya Dar es Salaam na Zanzibar pamoja na kuboresha zawadi za washindi, hongereni sana TMA”. Alisistiza Mhe. Mshibe.

“Lengo kuu la Tuzo hizi ni kuendelea kuleta hamasa na kujenga umahili katika uandaaji na usambazaji wa tarifa za hali ya hewa kwa jamii, na kuimarisha mchango wa wanahabari katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu na matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa”. Alieleza Dkt.Mshibe.


Akimkaribisha mgeni rasmi kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu, TMA, Dkt. Hamza Kabelwa, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri alisema Mamlaka kwa kutambua mchango huu mkubwa, imeendelea kuimarisha mahusiano haya kwa kuendelea kutoa motisha mbalimbali kwa wanahabari ikiwemo kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa takribani miaka 15 sasa hususani kipindi cha maandalizi ya utabiri wa mvua za misimu.

Comments