CCM YATAJA SABABU ZA USHINDI WAKE, YAWASHUKURU WANANCHI KWA KUWACHAGUA VIONGOZI WAKE



Na PrayGod Thadei,DAR

CHAMA cha mapinduzi CCM kimesema ushindi kilichoupata katika Uchaguzi wa serikali za mitaa ni dhihirisho la Imani ya watanzania kwa chama hicho.

Akizungumza katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo Lumumba Jijini Dar Es Salaam mbele ya waandishi wa Habari Leo Novemba 29,2024, Katibu wa NEC  itikadi,uenezi na mafunzo wa chama hicho Taifa, CPA Amos Makalla amesema kuwa baada ya kupata matokeo hayo Sasa ni muda wa Kazi.

Aidha amewashukuru watanzania kwa kukipa kura za ushindi chama hicho na amewataka wale wote walioshinda katika uchaguzi huo kuanzia ngazi za vijiji,vitongoji na mitaa kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha wanatekeleza vyema ilani ya chama hicho.

"Wale waliioshinda waliomba utumishi kwa wananchi na wananchi wakawachagua hivyo Sasa tunataka wawajibike kwa  wananchi pia ikiwemo kuomba barua kwa ajili ya shughuli zao mbalimbali pamoja na kufanya vikao vya mapato na matumizi kwa wananchi kama ilani yetu inavyosema"amesema CPA Makalla.

Hata hivyo amesema mafanikio yaliyopatikana katika uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na Serikali anayoiongoza ndiyo iliyochangia kupata ushindi huo kwa kishindo kwani wagombea wote walifanyiwa tathmini na chama na Kisha wakapitishwa na chama hicho hali iliyopelekea ushindi mnono.

Kuhusu migogoro ndani ya vyama vya siasa Makalla amesema migogoro hiyo ya vyama vya upinzani pia imesababisha CCM kushinda kutokana na wananchi kukosa Imani na vyama hivyo.

"Nyie mlishuhudia migogoro ikiwemo baina ya viongozi wao huyu akimtuhumu yule hivi na yule akimtuhumu huyu hivi na wengine wanatuhumiana kwa kukaa katika uongozi muda mrefu bila kumpisha mwenzake na siku zote hamuwezi kushinda kama una migogoro wapatane Sasa huko" amesema.

Amesema pamoja na ushindi huo pia Kuna vijiji ambavyo walikuwa katika uongozi kwa muda mrefu lakini kupitia uchaguzi huu baadhi yake vimeenda kwa upinzania na wao kama chama wanakubali kwani ndiyo demokrasia.

Kwa mujibu wa matokeo rasmi ya uchaguzi huo yaliyotangazwa jana na Waziri wa nchi ofisi ya Rais,TAMISEMI Mohamed Mchengerwa alitangaza matokeo ya jumla ya uchaguzi wa Serikali za mitaa, amesmea kuwa katika nafasi ya uenyekiti wa kijiji Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeongoza kwa asilimia 99.01 kikifuatiwa na Chadema.

Kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji ni 12,271 kati ya nafasi 12,280 zilizopaswa kufanya uchaguzi. Kati ya nafasi hizo, CCM imeshinda nafasi 12,150 sawa na 99.01%, Chadema imeshinda nafasi 97 sawa na asilimia 0.79% ACT Wazalendo imeshinda nafasi 11 sawa na 0.09% CUF imeshinda nafasi 10 sawa na 0.08%, NCCR Mageuzi imeshinda nafasi 1 sawa na 0.01% UMD imeshinda nafasi 1 sawa na 0.01% na ADC imeshinda nafasi 1 sawa na 0.01%.

Comments