MAMA ONGEA NA MWANAO 'YAMWAGA MISAADA KWA WENYE ULEMAVU DAR,WAMTAJA RAIS SAMIA








Dar es Salaam, Desemba 31, 2024 – Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Steven Mengele maarufu kama Steve Nyerere, imeshiriki katika kongamano maalum lililofanyika katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, kwa kutoa huduma za tiba na msaada kwa watu wenye mahitaji maalum na wakazi wa jiji hilo.

Mgeni rasmi katika kongamano hilo alikuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omari Kumbilamoto, ambaye alisifu juhudi za taasisi hiyo. Alitoa wito kwa jamii kuiga mfano wa Steve Nyerere katika kuunga mkono watu wenye ulemavu na makundi mengine yenye mahitaji maalum.

"Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, chini ya uongozi wa Steve Nyerere, imeonyesha mfano bora wa upendo na mshikamano kwa jamii kwa kutoa msaada wa vifaa mbalimbali. Ni jambo la kuigwa," alisema Kumbilamoto.

Aidha, Meya Kumbilamoto alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka mipango madhubuti ya kusaidia watu wenye ulemavu, ikiwa ni pamoja na kutenga shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kundi hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Steven Mengele, alisema kuwa taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia watu wenye mahitaji maalum tangu kuanzishwa kwake miaka mitatu iliyopita. Mwaka huu pekee, taasisi hiyo imetoa msaada wa viti vya magurudumu 25, jezi, na mipira kwa makundi mbalimbali.

“Rais wetu, Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameamua kushika mkono kundi hili maalum. Kupitia juhudi zake, taasisi yetu itatembelea mikoa mbalimbali nchini, ikitoa zawadi kama viti mwendo 50 na kukarabati madarasa ya shule za watoto wenye mahitaji maalum,” alisema Steve Nyerere.

Aliongeza kuwa lengo la taasisi hiyo ni kuhakikisha wahitaji wanapata msaada wa kutosha, huku akisisitiza umuhimu wa kushiriki nao kwa karibu, kusherehekea pamoja, na kujenga furaha ya pamoja.

“Nawashukuru wote mliohudhuria leo. Kupitia uongozi wa Rais wetu, taasisi ya Mama Ongea na Mwanao pia itasaidia vikundi vya vikoba vya watu wenye mahitaji maalum kwa kuwapatia shilingi milioni tano kwa kila kikundi,” alisema.

Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao imejipambanua kama mfano bora wa taasisi zinazosaidia jamii, ikichangia kwa hali na mali kuboresha maisha ya watu wenye uhitaji maalum kote nchini.

Comments