RC Chalamila Azungumzia Maendeleo ya Miundombinu, Huduma za Maji, na Usalama Jijini Dar es Salaam

 RC Chalamila Azungumzia Maendeleo ya Miundombinu, Huduma za Maji, na Usalama Jijini Dar es Salaam






NA MWANDISHI WETU 

 Mkuu wa Dar es Salaam, Bw. Albert Chalamila, ametoa taarifa kuhusu hatua kubwa zinazofanyika kuboresha miundombinu kupitia Mradi wa Kuboresha Maeneo ya Mijini (DMDP)awamu ya pili sambamba na hali ya usalama

RC Chalamila ameyasema hayo Leo Disemba 23,2024 wakati akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es salaam kuhusu matukio mbalimbali yaliyotikisa katika Mkoa huo kwa mwaka 2024 sambamba na salamu zake kwa wananchi kuelekea sikukuu za Krismasi na mwaka mpya

Amesema kuwa wakandarasi Mkoani humo wamepewa jukumu la kujenga barabara zenye urefu wa kilomita 255 pamoja na mifereji ya maji ya kilomita zaidi ya 90 katika maeneo mbalimbali ya jiji,MIRADI ambayo itachangia Kasi ya mendeleo.

RC Chalamila amesema miradi hiyo inatarajiwa kuanza rasmi mwezi Januari 2025, ikiwa na lengo la kupunguza changamoto za usafiri na kudhibiti mafuriko katika maeneo ya mijini.

Kuhusu huduma za maji safi jijini, Bw. Chalamila alieleza kuwa hali ya upatikanaji maji imeanza kurejea baada ya changamoto za muda mfupi zilizotokana na uchakavu wa miundombinu. Alisema kuwa Shirika la DAWASA linaendelea na juhudi za kuboresha huduma hiyo ili kuhakikisha kuwa wakazi wanapata maji kwa uhakika na kwa wakati.

Katika hotuba yake kwa waandishi wa habari, Bw. Chalamila aliwatakia wakazi wa Dar es Salaam heri ya Krismasi na Mwaka Mpya, akisisitiza umuhimu wa kusherehekea sikukuu hizi kwa amani na kufuata sheria. Alitoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha usalama wa watoto wao wakati wa msimu huu wa sikukuu.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alikemea vikali uvumi wa matukio ya utekaji ulioenea mitandaoni huku akitoa mfano wa tukio lililoripotiwa hivi karibuni eneo la Temeke, alisema kuwa madai ya mtoto kutekwa yalikuwa ya uongo, kwani uchunguzi wa polisi ulionyesha kuwa mtoto huyo alifariki dunia baada ya kutumbukia kisimani katika madrasa alipokuwa akisoma.

Aidha alieleza kuwa uvumi wa aina hiyo huleta taharuki isiyo ya lazima na kusisitiza umuhimu wa kupata taarifa za uhakika kabla ya kuzisambaza.

Kwa kumalizia, aliwasihi wakazi wa jiji hilo kushirikiana katika juhudi za maendeleo na kudumisha amani kwa maslahi ya wote. Alisisitiza kuwa maendeleo ya Dar es Salaam yanahitaji mshikamano wa kila mmoja katika jamii.

Comments