MKUTANO MKUU CCM HAUKUVUNJA KATIBA, MAAMUZI YOTE NI HALALI:WASIRA

 MKUTANO MKUU CCM HAUKUVUNJA KATIBA, MAAMUZI YOTE NI HALALI:WASIRA







DAR ES SALAAM.

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Stephen Wasira, amewataka wanachama na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutambua kuwa maamuzi yote yaliyofanywa na Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kuhusu uteuzi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kugombea kiti cha Urais yamezingatia misingi thabiti ya Katiba ya Chama.

Wasira amesema hayo jijini Dar es Salaam leo mbele ya wanachama wa CCM na wananchi waliokusanyika kumpokea, akieleza kuwa mamlaka ya Mkutano Mkuu hayana shaka, kwani ndio chombo cha juu zaidi katika mfumo wa uongozi wa chama.

"Katiba yetu inatuelekeza wazi kwamba Mkutano Mkuu unayo mamlaka ya mwisho ya kufanya maamuzi. Tulipomteua Dk. Samia, hatukupuuza utaratibu wowote. Kwa mujibu wa ibara ya 101 ya Katiba ya CCM, Mkutano Mkuu unawajibika kuteua jina moja la mgombea wa Urais," alisisitiza Wasira.

Ameongeza kuwa baadhi ya wanaojiita wanachama wa CCM ambao wanaonyesha mashaka juu ya uamuzi huo wanapaswa kuelimishwa ili waelewe vizuri maana ya utaratibu wa kikatiba wa chama.

"Kama kuna mtu hajui au hana uhakika, nawaomba wasiwe na hofu. Naweza kuwasaidia kuelewa maana katiba ipo kichwani mwangu. Hatuwezi kuwa na chama imara bila kufuata mwongozo wake," amesema.

Wasira ametoa wito kwa wanachama wa CCM kuendelea kuunga mkono maamuzi ya chama huku akieleza kuwa serikali inayoongozwa na Dk. Samia imefanya kazi kubwa, hatua iliyoharakisha uteuzi wake kama mgombea wa urais kwa kipindi kingine.

"Uamuzi huu si wa mtu mmoja, ni wa chama kupitia kikao chake kikuu. Wanaoshindwa kuelewa wanakaribishwa kwa darasa zaidi," alihitimisha.

#ccm #wasira #samiasuluhu #uchaguzi2025

Comments