Skip to main content

WASICHANA WAONGOZA MATOKEO YA MTIHANI KIDATO CHA PILI 2024

 

WASICHANA WAONGOZA MATOKEO YA MTIHANI KIDATO CHA PILI 2024


#KAZIINAONGEA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), limesema wasichana wameongoza kufanya vizuri katika mitihani wa Kidato cha Pili na wa Darasa la nne, kwa mwaka 2024.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dkt. Said Mohamed imeeleza kuwa,katika matokeo ya mtihani wa upimaji wa Kidato cha Pili yaliyotangazwa Jumamosi, Januari 4, 2025 na Baraza la Mitihani ya Taifa (NECTA), yameeleza kuwa, jumla ya wanafunzi 680,574 kati ya wanafunzi 796,825 waliofanya mtihani huo wamefaulu, sawa na asilimia 85.41.

Amesema,  wanafunzi hao wamefaulu kuendelea na kidato cha tatu kwa kupata madaraja ya I, II, III na IV, ambapo matokeo haya yanaonyesha kuwa, wasichana waliofaulu ni 367,457, ikiwa ni asilimia 54, huku wavulana wakiwa 313,117, sawa na asilimia 46.

Akielezea matokeo ya Mtihani kwa Darasa la Nne, Dkt. Mohamed amesema, jumla ya wanafunzi 1,320,227 kati ya wanafunzi 1,530,911 waliofanya mtihani wa Darasa la Nne, sawa na asilimia 86.24 wamefaulu kwa kupata madaraja A, B, C na D ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.9.

NECTA imesema kati ya waliofaulu, wasichana ni 699,901 sawa na asilimia 53, na wavulana ni 620,326 sawa na asilimia 47.

Takwimu zinaonesha kuwa jumla ya shule 197 kati ya shule 20,036 za Msingi zimepata wastani wa Daraja E katika mtihani wa Darasa la Nne, ikiwa ndilo daraja la chini zaidi lenye alama kati ya 0 na 60. 

NECTA imesema idadi ya shule zilizofanya vibaya zimepungua kwani mwaka 2023 zilikuwa 325.

“Wanafunzi wa kujitegemea waliofaulu upimaji na kupata sifa ya kufanya mtihani wa kidato cha nne ni 4,205 sawa na asilimia 55.94, huu ni mwaka wa kwanza kwa Wanafunzi wa kujitegemea kutahiniwa upimaji huu”

Mitihani ya Taifa ya kuwapima uwezo wanafunzi wa Kidato cha Pili na Darasa la Nne, ulifanyika mwezi Oktoba na Novemba, 2024 Tanzania nzima.

*#KAZIINAONGEA*

Comments