ACT Wazalendo Kujipanga kwa Ushirikiano Imara Ili Kukiondoa CCM Madarakani
ACT Wazalendo Kujipanga kwa Ushirikiano Imara Ili Kukiondoa CCM Madarakani
Na Mwandishi Wetu
Chama cha ACT Wazalendo kimeeleza dhamira yake ya kushirikiana na vyama vingine makini pamoja na wadau wa demokrasia nchini katika safari ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, lengo likiwa kuhakikisha Chama cha Mapinduzi (CCM) kinaondoka madarakani.
Kauli hiyo imetolewa leo, Februari 23, 2025, na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu, alipokuwa akifungua Mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho katika Makao Makuu yake, Magomeni, jijini Dar es Salaam.
Semu amesema kuwa kuelekea uchaguzi huo, changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni hujuma na hila zinazolenga kuwavunja moyo wananchi, lakini akasisitiza kuwa chama chake kimejipanga kusukuma mbele ajenda ya umoja wa kisiasa ili kuhakikisha ushindani wa kweli unapatikana.
"Tunapaswa kufanya kazi kwa pamoja kuimarisha mshikamano wetu, kwani huo ndio utakaotuletea ushindi. Hakuna uchaguzi wa kweli nchini mwetu—kinachoendelea ni uchafuzi wa uchaguzi," alisema Semu.
Akitilia mkazo hoja yake, alidai kuwa CCM haiwezi kushindana katika uchaguzi ulio huru na wa haki, na badala yake hutegemea mabavu, vipigo, kamatakamata, utekaji na hata mauaji ya wale wanaopinga wizi wa kura.
"Uchaguzi ni kama vita"
Semu aliweka wazi kuwa hali ya kisiasa nchini ni sawa na vita, akifananisha mchakato wa uchaguzi na mapambano yanayohitaji uthabiti wa viongozi na wanachama wa ACT Wazalendo.
"Katika vita kuna nyakati za ushindi na nyakati za changamoto. Kuna wakati wa kuendelea kupambana na pia wakati wa kupoteza baadhi ya mapambano. Lakini jemedari mzuri kamwe hakati tamaa—anajifunza, anajipanga na kuhakikisha anasonga mbele kwa nguvu mpya," alisisitiza Semu.
Akiwahimiza wanachama wa chama hicho, aliwataka kuwa tayari kukabiliana na hujuma zote zitakazojitokeza, huku wakidumisha mshikamano na uthabiti wa kisiasa.
"Iwapo sisi wenyewe tutakata tamaa, basi tutakuwa tumejitoa kwenye vita kabla hata ya kushindana. Hilo hatuwezi kulikubali!" aliongeza kwa msisitizo.
Kwa mujibu wa Semu, ACT Wazalendo inapaswa kujipanga kwa umakini ili kukabiliana na changamoto za kisiasa zinazoletwa na CCM na dola, huku wakitumia mbinu sahihi kuhakikisha wanatimiza malengo yao.
"Kwa mshikamano wetu, tunaweza kufanikisha malengo yetu na kuleta mabadiliko tunayoyahitaji. Ni wakati wa kuchukua hatua kwa pamoja na kupambana hadi haki ipatikane," alihitimisha Semu.





Comments