ADO SHAIBU: ACT WAZALENDO TUTAPIGANIA MABORESHO YA MFUMO WA UCHAGUZI
ADO SHAIBU: ACT WAZALENDO TUTAPIGANIA MABORESHO YA MFUMO WA UCHAGUZI
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Chama Cha ACT WAZALENDO kimetangaza maazimio yake kufuatia kikao chake Cha halmashauri kuu kilichokutana jana jijini Dar es salaam huku suala la kupigania mfumo Bora wa uchaguzi likitajwa kwa umuhimu mkubwa.
Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar Es Salaam wakati akitangaza maazimio ya kikao hicho,Katibu Mkuu wa chama hicho Ado Shaibu amesema Halmashauri Kuu ya Chama hicho imekutana katika kikao chake cha kawaida tarehe 23 Februari 2025, Makao Makuu ya Chama, jijini Dar es Salaam, ambapo ilijadili hali ya kisiasa nchini, vurugu za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, na mwelekeo wa chama katika kukabiliana na changamoto za uchaguzi.
Amesema kuwa baada ya mjadala wa kina, Halmashauri Kuu imeazimia hatua mbalimbali, zikiwemo kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi, kuchapisha ripoti za ukiukwaji wa haki za binadamu, na kuanzisha Operesheni Linda Demokrasia.
" Halmashauri Kuu imebaini kuwa maridhiano yaliyoahidiwa na Rais Samia Suluhu Hassan yamesambaratika, huku falsafa yake ya 4R ikielezwa kuwa imekosa utekelezaji wa vitendo. ACT Wazalendo imesema kuwa licha ya vyama vya upinzani kumuunga mkono Rais Samia katika ahadi yake ya kuboresha mazingira ya kisiasa, hakuna utashi wa kisiasa wa kutekeleza ahadi hizo" amesema
Ameongeza kuwa Kutokana na hali hiyo, chama kimemtaka Rais Samia kujitathmini juu ya utofauti uliopo kati ya ahadi anazotoa kwa maneno na utekelezaji wake wa vitendo ili kuendana na sera yake ya 4r.
Hata hovyo Halmashauri Kuu ya Chama hicho imeelekeza Chama kuandaa ripoti ya kina juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Ripoti hiyo itajumuisha matukio ya mauaji, utekaji, na madhila ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024.
Kwa upande wa Zanzibar, chama kimekusanya ushahidi wa mauaji ya raia 21 pamoja na matukio mengine ya ukatili wa kisiasa yaliyofanyika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2020. Ripoti hiyo itachapishwa na kuwasilishwa kwa wadau wa demokrasia, jumuiya ya kimataifa, na taasisi za fedha za kimataifa.
ACT Wazalendo imeeleza kuwa kipaumbele chake kwa sasa ni kuhakikisha maboresho ya mfumo wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na Kufanyika kwa mabadiliko madogo ya katiba (minimum constitutional reforms).
Kuundwa kwa Tume Huru za Uchaguzi kwa pande zote mbili za Muungano (NEC na ZEC).
Kupinga kwa nguvu zote kura ya mapema kwa upande wa Zanzibar.
Aidha, chama kimeazimia kushirikiana na vyama vingine vya upinzani, asasi za kiraia, na viongozi wa dini katika kujenga vuguvugu la kitaifa la kupigania mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.
Katika hatua nyingine, ACT Wazalendo imeelekeza kuanzishwa kwa Operesheni Linda Demokrasia ili kuhamasisha wananchi kupigania haki zao za kidemokrasia na kutokubali kunyimwa haki zao.
Chama kimewataka wanachama na viongozi wake kote nchini kujiandaa kwa ajili ya mapambano ya kulinda demokrasia.
"Muda wa kubembeleza mageuzi umekwisha, sasa ni muda wa mapambano!" alisema Ado
Kuhusu ushirikiano wa chama hicho na vyama vingine vya upinzani Ado amesema kuwa tayari wameshaviandikia barua vyama vya CUF,ADC,NCCR MAGEUZI na CHADEMA kuomba kishirikiana navyo katika masuala mbalimbali kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.



Comments