RC CHALAMILA KUSHUHUDIA KNOCK OUT YA MAMA DAR,MAFIA BOXING 'YAMWAGA'MITUNGI YA GESI KWA AKINA MAMA MAGOMENI
RC CHALAMILA KUSHUHUDIA KNOCK OUT YA MAMA DAR,MAFIA BOXING 'YAMWAGA'MITUNGI YA GESI KWA AKINA MAMA MAGOMENI
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, anatarajiwa kushuhudia mapambano ya ngumi yasiyo ya kuwania mkanda leo, Februari 28, katika Ukumbi wa Magomeni Sokoni.
Taarifa zinasema Chalamila atakuwa miongoni mwa viongozi watakaohudhuria tukio hilo.
Katika utambulisho wa mabondia hao, hali ya mvutano ilizuka kati ya Abdallah Pazzy ‘Dullah Mbabe’ na mpinzani wake, ambapo walionekana kutaka kuzichapa kabla ya muda rasmi wa pambano lao. Tukio hilo liliongeza msisimko kwa mashabiki wa masumbwi.
Pambano linalosubiriwa kwa hamu ni kati ya Amiri Matumla, mtoto wa bingwa wa zamani Rashid Matumla ‘Snake Man’, dhidi ya bondia kutoka Namibia, Pauls Amavila. Hili litakuwa pambano kuu la usiku huo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mafia Promotion, Ally Zayumba, kutakuwa na mapambano 14 yatakayoshirikisha mabondia wa ndani na nje ya nchi, yakiwa sehemu ya msimu wa tatu wa mashindano ya "Knockout ya Mama".
Zayumba amesema lengo kuu la mashindano haya ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza michezo na kutangaza miradi ya Serikali ya Awamu ya Sita, ikiwa ni moja ya jitihada za kukuza mchezo wa ngumi nchini.
Mabondia walipima uzito Februari 27 asubuhi kabla ya utambulisho rasmi wa pambano lao. Viingilio kwa mashabiki wa ngumi ni Sh 50,000, Sh 20,000, na Sh 10,000 kulingana na sehemu ya ukumbi.
Katika hatua nyingine, Mafia Boxing Promotion imegawa majiko ya gesi kwa Mama Ntilie zaidi ya 30 wa Magomeni Sokoni, ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono Rais Samia katika kupunguza matumizi ya nishati chafu kama mkaa na kuni.
Mama Ntilie waliopokea majiko hayo wameishukuru Mafia Boxing Promotion kwa msaada huo, wakisema utawasaidia kupika haraka na kuongeza ufanisi katika biashara zao.
Comments