TANZANIA YATAJWA KAMA MWENYEJI WA KONGAMANO LA MAFUTA NA GESI 2025,KUWAVUTIA WAWEKEZAJI
TANZANIA YATAJWA KAMA MWENYEJI WA KONGAMANO LA MAFUTA NA GESI 2025,KUWAVUTIA WAWEKEZAJI
DAR ES SALAAM.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, ametoa wito kwa Watanzania kutumia Kongamano la 11 la Mafuta na Gesi la Afrika Mashariki kama fursa ya kutangaza rasilimali za nishati zinazopatikana nchini ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya kongamano hilo linalotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, Mhandisi Mramba alibainisha kuwa mkutano huo utafunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. Kongamano hilo litafanyika chini ya kaulimbiu isemayo: "Kufungua Fursa za Uwekezaji katika Nishati: Mchango wa Rasilimali za Mafuta katika Kufanikisha Upatikanaji wa Nishati Endelevu kwa Maendeleo ya Afrika Mashariki."
Mhandisi Mramba alisisitiza kuwa Tanzania ni moja ya nchi zenye utajiri mkubwa wa gesi asilia, lakini bado haijatumia kikamilifu fursa hiyo kwa maendeleo ya uchumi wa taifa. Alisema kongamano hilo litatoa jukwaa muhimu la kujadili namna bora ya kutumia rasilimali hizo ili kufanikisha malengo ya bara la Afrika ya kuwapatia umeme zaidi ya watu milioni 300 ifikapo mwaka 2030.
"Kwa sasa dunia inahama kutoka kwenye nishati chafu kama makaa ya mawe na mafuta mazito kwenda kwenye nishati safi kama gesi asilia. Tanzania iko kwenye nafasi nzuri ya kuchangia katika mabadiliko haya na tunapaswa kutumia kongamano hili kujifunza na kujiimarisha," alisema Mramba.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya EAPC’E25, Dkt. James Mataragio, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia sekta ya mafuta na gesi, alisema kongamano hilo litaleta pamoja wataalamu wa sekta hiyo, wawekezaji, na wadau muhimu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki.
"Zaidi ya washiriki 1,000 kutoka nchi nane za ukanda wa Afrika Mashariki wanatarajiwa kuhudhuria. Mkutano huu utajadili changamoto zinazoikabili sekta hii, pamoja na mbinu za kuzitatua kwa manufaa ya mataifa yetu," alisema Dkt. Mataragio.
Tanzania imekuwa ikihimiza uwekezaji katika sekta ya gesi asilia, hasa kwa kuzingatia miradi mikubwa inayoendelea kama mradi wa kuchakata gesi asilia kimiminika (LNG) unaokadiriwa kugharimu takriban dola bilioni 42. Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa sekta hiyo wanahoji kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo na changamoto za kisheria zinazoweza kuathiri uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje.
Pamoja na matarajio makubwa, wadau wanapendekeza kuwa kongamano hili lisibaki kuwa jukwaa la mijadala tu, bali litoe mwongozo wa wazi kuhusu mikakati ya muda mfupi na mrefu ya kuhakikisha Tanzania inanufaika ipasavyo na utajiri wake wa mafuta na gesi.
Comments