TLP KUANZA 'KUVUNA' WANACHAMA NCHI NZIMA,LYIMO ASEMA WAMEJIPANGA
TLP KUANZA 'KUVUNA' WANACHAMA NCHI NZIMA LYIMO ASEMA WAMEJIPANGA
Chama Cha Tanzania Labour Party (TLP) Kinatarajia kuanza mchakato wa kuongeza idadi ya wanachama wake nchi nzima ambao watakisaidia chama hicho kupata kura za kutosha katika uchaguzi mkuu wa madiwani wabunge na Rais unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa Chama hicho,Taifa Richard Lyimo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari waliomtembelea ofisini kwake,Makao makuu ya Chama Magomeni, Jijini Dar Es Salaam ili kujua mipango ya chama hicho mara baada ya kumalizika uchaguzi wa viongozi wake wa kitaifa.
Lyimo alisema kuwa ili kuanza kwa mchakato huo wataanza kwa kuandika waraka katika Mikoa yote kuhakikisha nafasi za viongozi kuanzia ngazi za Wilaya na Mikoa zilizo wazi zinajazwa ili kuanza mchakato wa kupata wanachama.
"Tumeona kwamba tukijaza nafasi zote za uongozi na Kila Mkoa kiongozi wetu akawajibika vizuri na kuwa na viongozi ambao wanatosheleza nia yetu ni kwamba hauwezi kuwa na wanachama ambao wanajitosheleza kama huna viongozi wa kuwasimamia na kuwatafuta Sasa makao makuu haiwezi kuzunguka Mikoa yote kwenda kutafuta wanachama tukagundua kuwa ni vyema Sasa Mikoa yetu tuipe nguvu na Kazi za kufanya na sisi tutawatembela kujua walipofika" amesema Lyimo.
Aidha aliongeza kuwa kuwa endapo chama hicho kitaongeaza idadi kubwa ya wanachama,Hali hiyo itapelekea pia wagombea watakaotia nia waweze kuamini kwamba wakigombea kwa chama hicho wanaweza kushinda katika nafasi mbalimbali ikiwemo Ubunge,udiwani na nafasi ya Urais.
"kwa hiyo Kazi yetu ni kuandaa mazingira mazuri ya wagombea Ubunge na udiwani na hata nafasi ya Urais Kutokana na kuimarika kwa chama ili kuwashawishi nao wagombea wakiamini kwamba wanachama waliokwisha andaliwa wapo wa kutosha kukipa chama ushindi" amesisitiza Lyimo.
Kuhusu chama hicho kuungana na vyama vingine vya upinzani kuelekea uchaguzi mkuu kikiwemo chama Cha ACT Wazalendo ambacho kimesema kinataka kuungana na ADC,CUF,NCCR na Chadema Lyimo alisema kuwa kwa sasa chama TLP hakiko tayari kwa Sasa kwani miungano ya vyama mara nyingi Huwa Haina faida na hufaidisha chama kimoja.
"Suala la vyama kutaka kuungana nimelisikia na kwa sababu Mimi ni mzoefu wa siasa na siyo mara ya kwanza kwa vyama hivi kusema kuungana,tushaungana miaka ya nyuma tukafika katikati muungano ule ukafa kwa sababu tuu ilionekana chama kimoja kinavizia watoto wa chama kingine,kilichoko kwenye muungano kwa kupitia muungano huo huo,na tukakaa tukauliza na moja kati ya watu waliotendewa ni Lipumba ambaye wagombea wake walichukuliwa na chama hicho tena wakati wanagombea"alisema Lyimo.
Aliongeza kuwa hata baada ya kuja kwa Ukawa ambao ulitokana na muungano wa kudai katiba ambao baadaye ulibadilika na ikawa ni sehemu ya Mkakati wa kushinda kwa vyama vilivyoungana wakati huo na hiyo ilipekekea chama kimoja kunufaika zaidi na umoja huo kuliko vingine na pia waliwekeana wagombea katika sehemu ambazo ilibidi waweke mgombea mmoja ili washinde hivyo baadhi ya vyama vilijiondoa kwenye umoja huo kwa Kuona kuwa havikupata thamani inayostahili.
"hakuna faida yoyote waliyopata wale walioungana na Chadema kushiriki kwenye uchaguzi,badala yake wao walipata hasara ya kuvimaliza vyama vyao na kujidhalilisha,Sasa unapozungumza tena Leo twende tukaungane Mimi napata mashaka kwa sababu wanaosema tuungane,Kila mmoja amemaanisha kwamba tuungane kwa maana ya mumuunge mkono na usipomuunga mkono huo muungano hautaki" amesema na kuongeza kwamba,
"Mimi siyo kwamba nauchukia muungano hapana wa vyama hapana napenda sana muungano lakini kwa Tanzania,havijatokea vyama vyenye uwezo wa kufanya muungano wa kweli kwa maana ya kuiondoa Serikali na kwa kuwa Mimi naelewa hivyo,siwezi kukipeleke chama changu"
Awali akilitolea ufafanuzi kuhusu taarifa ambazo ziliripotiwa na baadhi ya vyombo vya Habari kuwa msajili wa vyama vya siasa alikiandikia chama hicho barua ya kujieleza ndani ya siku zisizopungua saba kuhusu uchaguzi wa vioongozi wake uliofanyika siku chache zilizopita ambayo ilitolewa na aliyewahi kuwa katibu mwenezi wa chama hicho,Geofray Stephen ambaye alifukuzwa na kufutwa uanachama ndani ya chama hicho Lyimo alisema taarifa hizo ni za uongo na zinalenga kupotosha umma na hakuna barua yoyote waliyoandikiwa kutoka ofisi ya msajili wa vyama.
Lyimo aliongeza kuwa amesikitishwa sana na taarifa hiyo ambayo haina ukweli wowote iliyotolewa kwenye vyombo vya Habari likiwemo gazeti moja maarufu ambalo lilichapisha habari hiyo bila kupata udhibitisho kutoka ndani ya chama hicho na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.
"nimeona gazeti moja kubwa limeandika habari hiyo,kwanza hatuna malalamiko ya aina yoyote Wala hatujawahi kupata barua kutoka kwa msajili wa vyama vya siasa na hao walioandika walipaswa kutuuliza kwanza kabla ya kupotosha umma" alisema
Aliongeza kuwa chama hicho barua kilichokuwa nayo ni ya msajili ambaye alipinga madai ya wanaojiita wanachama wa TLP,huku wakiwa hawana uhalali wa kupeleka malalamiko hayo kwani siyo wanachama na walishafukuzwa na hata kwenye mkutano mkuu uliouchagua uongozi ulio madarakani hawakuwepo na kwamba mkutano huo ulikuwa halali na msajili wa vyama vya siasa anautambua.
Comments