ADOLESCENCE ,SERIES AMBAYO ITAKUACHA MDOMO WAZI,HII HAPA KWA UFUPI.
ADOLESCENCE ,SERIES AMBAYO ITAKUACHA MDOMO WAZI,HII HAPA KWA UFUPI.
Asubuhi, familia ya watu wanne, katika mtaa f’lani wa kishua, inaamshwa na kishindo cha polisi, walioutandika mlango kwa gongo la Fatuma.
Mlango ulipoachama Waaa! Wakaingia mkukumkuku silaha mkononi.
Mama akalala kifudifudi sakafuni, baba akainua mikono juu huku akijaribu kuwaambia polisi, hajafanya chochote kibaya, yawezekana wamekosea nyumba.
Ukiondoa yeye na mkewe, familia ya bwana Miller ina watoto wawili; binti mkubwa, Lisa, ambaye balehe bado haijamkauka maungoni, na kijana wa kiume, Jamie, ambaye ndiyo kwanza ana miaka 13.
Polisi walioingia wanampita Bwana Miller aliyekuwa amesimama kwenye ngazi, wao wanaelekea ghorofani, huku wakimwamrisha kubana hapo ukutani.
Miller anabumbuazika, kama si yeye wala si mkewe, anayesakwa na polisi, watakuwa wanamtaka nani?
Polisi wanagawana vyumba vya kuingia, walioingia chumba cha Jamie wanatoa taarifa kuwa wamempata mtuhumiwa. Hapo Jamie anaamrishwa kuweka mikono juu na kujulishwa yupo chini ya ulinzi.
Kule kwenye ngazi, Miller anaambiwa kuna search warrant ya makazi yake, anaulizwa kijana wako yuko wapi? Anajibu yupo chumbani. Mama wa familia analalamika kuwa polisi wamekosea nyumba. Baba anahoji wanamtakia nini kijana wake. Ni mtoto tu, ni mtoto tu huyo.
Askari Mpelelezi anapofika chumbani kwa Jamie anamjulisha kuwa anamweka chini ya ulinzi kwa tuhuma za mauaji.
Eeh, mauaji? Wazazi wake wanapayuka kuwa haiwezekani, itakuwa wamekosea nyumba. Hata ingekuwa ni wewe, polisi wanafika kwako kumkamata mtoto wako wa miaka 13 kwa tuhuma za mauaji, ilhali amelala hapo nyumbani, lazima ungewafungia kibwebwe.
Kelele za baba zinapozidi polisi anamuonya. Jamie anamwambia baba yake sijafanya chochote kibaya. Namna mvulana huyu mdogo anavyomwita baba yake na kujitetea kuna hali fulani ya huzuni unaweza kuihisi. Anapoamrishwa kuinuka toka kitandani, polisi anagundua Jamie amejikojolea.
Jamie anachukuliwa, baba yake anauliza hili na lile kama mkuu wa familia. Wanapoambiwa anapelekwa kituoni kwa tuhuma hizo, wazazi wanakataa huku wakilalamikia zaidi nguvu iliyotumika kumkamata mtoto wa miaka 13.
Kule kwenye gari la polisi, Jamie anamwita baba yake kwa huzuni, baba anazidi kuchanganyikiwa. Anamtetea mtoto wake kadiri ya uwezo wake huku akimtia moyo.
Kituoni, Jamie anafuata taratibu zote. Mwanasheria pia anafika. Jamie anapotakiwa kutoa password ya simu yake anakataa, na halazimishwi. Baba yake anapopata wasaa wa kuongea na mwanasheria, baba huyu analia machozi ya uchungu. Anamuuliza mwanasheria, afanyeje sasa? Sehemu hii inaumiza nafsi, unapomwona baba ambaye ameumizwa mno na papo hapo anatakiwa aonyeshe ujasiri akiwa mbele ya mkewe, bintiye na kijana wake.
Tufupishe...
Ulifika wakati ambao wapelelezi, mwanasheria, Miller na Jamie walikaa meza moja kuzungumza. Maswali mengi ya msingi Jamie alijibu No comment. Yale yaliyohusu mapenzi na ngono kabla hata ya kujibu baba yake alikuja juu na kuhoji wanawezaje kumhoji mtoto wa miaka 13 maswali kama hayo?
Ndipo sasa, ikasemwa wazi, Jamie anatuhumiwa kumuua mwanafunzi mwenzake aitwaye Katie.
Jamie akaulizwa maswali kuhusu Katie. Akaulizwa maswali kuhusu akaunti yake ya Instagram ambayo hajiposti yeye ila anapost wanawake waliovalia nusu utupu. Akaunti ambayo hata baba yake haijui.
Akaulizwa alipokuwa usiku uliopita. Akaulizwa kama amemuua Katie, Jamie akakataa na baba akasikitika mtoto wake kuulizwa hivyo, na kupewa tuhuma nzito kama hiyo.
Mwishowe, Jamie, mwanasheria wake na baba yake wakawekewa video ya CCTV kutoka eneo la mauaji. Unajua nini, alichokiona Miller kwenye video ile kilimtoa machozi. Kilifungua safari nyingine ya maumivu makali mno.
Yaliyofuata, yalifumua mengine makubwa yaliyokuwa yanaendelea shuleni anakosoma Jamie.
Tuishie hapo....
- Series hii imezua mijadala mikubwa sana ya kila namna kuhusu watoto, vijana, misogyny (chuki dhidi ya wanawake), na mitandao ya kijamii, presha za makundi wanayokutana nayo shuleni na mitandaoni nk.
- Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer ameizungumzia hii series kwa hisia, kiasi cha kuipendekeza itazamwe shule za sekondari ili kuibua mijadala zaidi kwa vijana na mambo yanayoendelea miongoni mwao.
- Series hii inaweza kukuonyesha kwa kiasi gani malezi ya sasa yalivyo magumu sana tena sanaaa, hususani nyakati hizi zenye mitandao ya kijamii. Unaweza kujitahidi mno kulea, na kuna namna unaweza kudhani unawajua watoto wako vizuri sana, ukaamini bado wana akili ya kitoto, ukawaona ni watoto wema na wasikivu kwa sababu wanakuigizia wema na utulivu wanapokuwa mbele yako.
- Series hii inafikirisha zaidi kwa Miller ambaye alipita mikononi mwa baba mkali sana ambapo yeye aliapa kutokuwa hivyo. Aliapa kuwa bora zaidi, lakini kwa tukio la mtoto wake, Miller alijikuta katika msongo mpya, alijilaumu licha ya kuombwa asijilaumu. Kwamba alikosea wapi? Swali lake ndilo wengi tunajiuliza, wengi tunaposimulia malezi ya zamani tunaongelea aina fulani ya malezi yaliyotufanya kuwa imara, lakini huo uimara wetu haujaweza kuleta kizazi imara, tunacho kizazi hiki tunakiongelea vibaya mno. Kwa nini?
- Series hii inaonyesha namna mitandao ya kijamii inaweza kutuathiri vibaya sana. Si watoto tu hata sisi watu wazima. Leo hii tuna posts, tuna podcasts, tuna groups nk. ambazo zinasifia mauaji ya wanawake au wanaume hata kwa utani.
Ni kawaida kuona comments zinazohalalisha ukatili kama sehemu ya adhabu na mizaha. Hujaona watu wakitishiana kulawitiana kama adhabu? watu wakisifia mauaji ya wanawake kwa kusema wakome, wakisifia mauaji ya wanaume kwa kusema wamezidi, kwa kutamka ukipata nafasi ya kumuuza mwanamke au mwanaume fanya hivyo... Kuna watoto, kuna vijana wadogo wenye akili teke wanasoma haya, wanayaweka akilini. Kisha, tunapoanza kuona watoto wakifanya matukio ya kutisha TUNASHANGAA!!
- Series hii inatukumbusha wazazi na walezi, kuna dunia nyingine nje ya malezi unayompa mtoto wako. Kuna maongezi inabidi tuanze kuyafanya na watoto wetu.Tunakoelekea ni pa hatari zaidi. Hofu haisaidii, kuogopa mijadala haisaidii, kufunika chini maongezi yanayokutisha haisaidii. Dawa ni kuanza kuyakabili matatizo kwa sababu hatuwezi tena kuishi zama za zamani. Hatupo huko tena.
- Nyumbani tunaweza kuwafuatilia wanafanya nini kwenye simu, wanajiunga makundi gani, wanaongea na nani, wanatazama nini, lakini je huko shuleni na mtaani tunaweza kuwazuia wasitazame au wasisikie vitu tunawavyochunga kupitia makundi, marafiki kompyuta, au simu za wengine?
- Ni series inayoonyesha mchuma janga hula na wa kwao. Familia ya Miller ilibaki katika huzuni kubwa. Bwana Miller alipitia msongo mkali sana kiasi cha kuwaka hasira kila wakati. Hali kadhalika, matukio kama hayo huleta watu wanaotujadili katika namna yenye kutibua maumivu- bullies.
- Ni series inayofikirisha kuhusu balehe za wakati huu ambao kila kitu kiko mitandaoni. Elimu na maarifa yaliyo mazuri na mabaya yapo wazi sana.
- Kuna hizi challenge za ajabu mitandaoni, tunawaandaa vipi watoto wetu kuzipokea na kuzipembua? Kwa sababu nje ya nyumba ni dunia kamili yenye mengi sana. Sisi walezi tunaelewa vizuri dunia imetobokea wapi?
Zaidi, mhusika mkuu, Owen Cooper, aliyecheza kama Jamie Miller, si mwigizaji mzoefu wala si maarufu ila kipaji alichokionyesha humo ndani ni kikubwa sana. Unaweza kumtazama kwa wasiwasi kuwa huenda kweli ana tabia alizozionyesha wakati akizungumza na mwanasaikolojia. Amefanya kazi ngumu mno.
Adolescence ni series nzuri ukiamua kuitazama kama namna ya kujifunza kitu. Inafikirisha sana! Balehe za enzi hizo si za sasa aisee!
Laura Pettie
April, 2025
Nje ya Mji



Comments