CHALAMILA AHIMIZA AMANI DAR,WATAKAOVURUGA KUKIONA, azungumzia maendeleo ya Jiji hilo
CHALAMILA AHIMIZA AMANI DAR,WATAKAOVURUGA KUKIONA, azungumzia maendeleo ya Jiji hilo
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewahimiza wananchi, taasisi na vyama mbalimbali kufuata sheria na taratibu zilizowekwa katika kutafuta haki zao, badala ya kuandaa vurugu zisizo na tija kwa taifa. Amesema amani ya Tanzania imejengwa kwa muda mrefu kwa ushirikiano kati ya Serikali na wananchi, na haitavumiliwa kuvurugwa kwa namna yoyote ile.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya Mkoa huo, RC Chalamila ameuhakikishia umma kuwa Dar es Salaam ni salama na hakuna viashiria vya vurugu, hivyo mazingira ya uwekezaji na biashara yako shwari na yanaendelea kuimarishwa.
Kwa upande wa miundombinu, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo maalum ya kuanza kwa ujenzi wa daraja la juu eneo la Magomeni Fire, ili kupunguza msongamano wa magari na kuboresha usafiri jijini.
Aidha, amewasihi wakazi wa jiji hilo kulipa kodi kwa hiari ili kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wakati.
Kuhusu mradi wa barabara za mwendokasi awamu ya nne, unaojengwa kwa zaidi ya kilomita 30, RC Chalamila amesema Serikali iko katika hatua ya kuongeza ushirikiano na wadau wa maendeleo na kuongeza idadi ya mabasi ya mwendokasi ili kupunguza usumbufu kwa wananchi.
Ameeleza kuwa mkoa uko tayari kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kutekeleza ajenda ya Rais Samia inayojulikana kama 4R (Reconciliation, Resilience, Reforms and Rebuilding), hususan kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa Soko la Kariakoo, amesema ujenzi huo umefikia zaidi ya asilimia 95 na kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 28. Zaidi ya wafanyabiashara 1,500 tayari wamesajiliwa kwa ajili ya kurejea sokoni humo.
Kuhusu mpango wa biashara saa 24, RC Chalamila amesema utekelezaji wake unaendelea maeneo ya Kariakoo, Mwenge, Ubungo na kwingineko, na amewataka wakuu wa wilaya kuhakikisha uzinduzi rasmi wa mpango huo unafanyika na maeneo maalum yanatengewa.
Amesisitiza kuwa Dar es Salaam inaendelea kuwa kitovu cha biashara, maendeleo na fursa lukuki, huku Serikali ikiweka mazingira rafiki kwa wawekezaji, wafanyabiashara na wananchi.
Mwisho, amewatakia Wakristo na wakazi wote wa Jiji la Dar es Salaam Pasaka njema, akiwahimiza kusherehekea kwa amani, mshikamano na upendo mnamo Jumapili, Aprili 20, 2025.




Comments