Skip to main content

CHAMA CHA SAU CHAFANYA MKUTANO MKUU,AMANI YASISIZWA KUDUMISHWA NCHINI.


CHAMA CHA SAU CHAFANYA MKUTANO MKUU,AMANI YASISIZWA KUDUMISHWA NCHINI. 





NA MWANDISHI WETU 

CHAMA cha Sauti ya Umma (SAU) kimesema kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu kitafanya Kampeni za kistaarabu ili kutunza na kulinda Amani iliyopo Nchini.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 28, 2025 na Mwenyekiti wa Chama hicho Bertha Mpata akifungua Mkutano Mkuu wa Chama hicho uliokuwa na lengo la kufanya Uchaguzi wa viongozi wa Chama, kufanya mabadiliko ya Katiba na kupitisha wagombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa upande wa Zanzibar.

Mpata amewataka wanachama wa Chama hicho na Watanzania kutosikiliza Sauti za wanasiasa wanaotaka kuvuruga Amani na kuwagawa Watanzania.

"Sisi kama SAU tunapenda Amani, hivyo tunapokwenda kwenye Uchaguzi Mkuu, mtumie Sera zenu vizuri, msisikilize Lugha za matusi," amesema Mpata.

Mpata ameeleza kuwa kama Chama cha SAU hawafurahishwi na Lugha za kumtukana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwamba wanachukizwa na hali hiyo, huku akieleza kama Chama wanaunga mkono kazi Nzuri ambayo Rais Samia anafanya, hivyo ametoa rai aachwe afanye kazi yake.

"Kama SAU hatutafanya vurugu, hatuna sera ya matusi, hivyo tutajikita sisi kutangaza Sera zetu," amesisitiza Mpata.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa SAU Zanzibar Issa Mohamed Zonga amesisitiza kuhusu suala la kulinda Amani ya Nchi.

Naye Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa Sisty Nyahoza amesisitiza vyama vya Siasa kuhakikisha vinatunza Amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu.

Kwamba kipindi cha michakato ya Uchaguzi Mkuu kutokana na ushindani baina ya vyama, wanasiasa wamekuwa Wakati mwingine wakifanya mambo nje ya utaratibu na hivyo kuhatarisha Amani.

Hivyo amesema kwamba pamoja na azma ya kila Chama kutaka kushika Dola, vinapaswa kulinda Amani na sio vinginevyo.

Comments