DKT MPANGO MGENI RASMI TUZO YA TAIFA YA MWL NYERERE YA UANDISHI BUNIFU
NA MWANDISHI WETU
Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ni mojawapo ya nyenzo muhimu zinazotumika kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili, maarifa, na utamaduni wa taifa.
Tuzo hii si tu kwamba inaheshimu mchango mkubwa wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika nyanja ya elimu na lugha, bali pia inatoa fursa kwa waandishi – chipukizi na wakongwe – kuonyesha ubunifu wao kupitia kazi za fasihi kama riwaya, ushairi, hadithi za watoto na tamthiliya. Kwa kupitia tuzo hii, serikali inathibitisha dhamira yake ya kukuza vipaji na kuhimiza matumizi ya Kiswahili kama chombo cha maarifa na maendeleo ya kijamii.
Aidha, Tuzo hizi zimekuwa chachu ya kuinua hadhi ya uandishi wa kazi za fasihi nchini, kwa kuwapa waandishi motisha ya kutunga kazi bora na zenye maudhui ya kuelimisha, kuburudisha na kuhamasisha jamii. Kupitia tuzo hizi, maandiko bora huweza kufikishwa kwa jamii pana kupitia machapisho, hususan katika shule na maktaba, hivyo kusaidia kujenga jamii inayothamini kusoma na kuandika. Tuzo ya Mwalimu Nyerere si tu jukwaa la kuthamini ubunifu bali pia ni urithi wa fikra za Mwalimu unaoendelezwa kwa vitendo
Kwa kutambua hilo hatimaye Ile hafla ya utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2025 inatarajiwa kufanyika Aprili 13 katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 7, 2025 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo amesema Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Prof. Mkenda amesema kuwa maandalizi ya hafla hiyo yamekamilika na kwamba ni heshima kubwa kwa Sekta ya Elimu kuwa na ugeni huo wa juu unaoonyesha namna ambavyo serikali inatambua mchango wa uandishi bunifu katika kukuza lugha ya Kiswahili, maarifa, na utamaduni wa taifa.
Amesema kuwa Tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ni miongoni mwa njia bora za kuenzi fikra, falsafa na maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye aliweka msingi wa matumizi na ukuzaji wa lugha ya Kiswahili kama nyenzo ya elimu, umoja na maendeleo ya jamii ya Watanzania.
“Tuzo hii ni heshima kwa Mwalimu Nyerere lakini pia ni jukwaa mahsusi kwa waandishi chipukizi na wakongwe kuonyesha umahiri wao katika nyanja mbalimbali za uandishi kama vile riwaya, ushairi, hadithi za watoto na tamthiliya,” amesema Prof. Mkenda.
Waziri Mkenda ameleza kuwa katika hafla hiyo, washindi wa Tuzo kwa kila kundi watatangazwa rasmi, na zawadi zitakazotolewa zitajumuisha fedha taslimu, vyeti na kuchapishwa kwa kazi za washindi wa kwanza ambazo zitasambazwa katika shule na maktaba mbalimbali nchini kupitia ushirikiano na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Profesa Penina Mlama amesisitiza kuwa majaji wamekamilisha kazi ya kusoma miswada iliyowasilishwa na tayari orodha teule ya waandishi waliopendekezwa imechapishwa.
Ameeleza kuwa washindi wa mwisho watachaguliwa kutoka kwenye orodha hiyo teule.
Prof. Mlama alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha Watanzania wote kuhudhuria hafla hiyo ya kihistoria, huku akitoa shukrani kwa waandishi wa habari kwa mchango wao mkubwa katika kuutangazia umma juu ya umuhimu wa Tuzo hii tangu kuanzishwa kwake mwaka wa fedha 2022/23.
- Get link
- X
- Other Apps



Comments