MABONDIA WAFANYA 'SPARING' KUJIANDAA NA KNOCK OUT YA MAMA MSIMU WA 4 DAR

MABONDIA WAFANYA 'SPARRING' KUJIANDAA NA KNOCK OUT YA MAMA MSIMU WA 4 DAR




Kuelekea pambano la Knock out ya mama msimu wa 4 litakalopigwa May 25 mwaka huu,mabondia mbalimbali wamepimana uwezo kwa kufanya mazoezi ya kupigana baina ya washirika wawili  kwa lengo la kujifunza mbinu, kuimarisha ujuzi, kasi, na ustadi wa mapambano halisi,(sparring) itakayowawezesha kushiriki pambano hilo kubwa Afrika mashariki.

Sparing hiyo imefanyika April 26,2025 katika eneo la kufanyia mazoezi (gym) ya kampuni ya Mafia boxing Promotion iliyopo katika Mtaa wa  Mbezi,Msumi pembezoni mwa hifadhi ya msitu wa pori la Pande,nje kidogo ya Jiji la Dar Es Salaam.

Wakizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kumalizika kwa sparing hiyo baadhi ya mabondia walioshiriki sparing hiyo  wamesema kuwa mazoezi hayo  yamewajengea uwezo kimapambano kuelekea katika pambano kubwa la Knock out ya mama msimu wa 4  litakalopigwa katika viwanja vya Posta,Kijitonyama.

Haidary Mchanjo ni bondia wa kujitegemea wa ngumi za kulipwa nchini Tanzania ambaye aliwaambia waandishi wa Habari kuwa kupitia mazoezi hayo wamepeana changamoto mabondia mbalimbali kutoka kampuni ya Mafia boxing na wale ambao wanajitegemea na wanaotoka kampuni nyingine.

Mchanjo amesema kuwa hapo awali mchezo wa ngumi ulionekana kama ni mchezo wa wahuni lakini baada ya serikali ya awamu ya sita kupitia Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan  kuuheshimisha mchezo huo kwa Sasa jamii imeanza kuuchukulia kama mchezo rasmi na kazi ambayo unawaingizia kipato wapiganaji.

"Kuelekea knock out ya mama sisi kama mabondia pia tumefurahi kwa jinsi mheshimiwa Rais anavyojitoa kwetu na kutuunga mkono kupitia mchezo wa ngumi na zawadi yake aliyotoa kwetu na mimi niliipata hivyo amekuja kutia morali kwetu na sisi tutaliwakilisha vyema Taifa letu" alisema Mchanjo.



Kwa upande wake bondia kutoka kampuni ya Mafia boxing Promotion Mchanja Yohana maarufu kama (computer master) alisema kuwa mchezo wa masumbwi kwa sasa hapa nchini umeendelea kuwa ni miongoni mwa michezo pendwa kwa watanzania kutokana na kupewa heshima inayostahili kwa sasa hivyo kwa kufanya mazoezi hayo ya pamoja baina ya mabondia mbalimbali nchini itawajengea uwezo mkubwa kimapambano.

Ameishukuru kampuni ya Mafia boxing kwa kuamua kuwaweka pamoja mabondia kupitia mazoezi (sparing) na kuahidi kumchapa mpinzani ambaye atakutana naye kwenye pambano la Knock out ya mama ambalo linatarajiwa Kupigwa hivi karibuni.

"sparing imenipa mazoezi makubwa sana kuelekea pambano langu kwani Leo nimejipima utimamu wa mwili,akili na mapafu na niko vizuri hivyo naamini ulingo utawaka moto"alisema Mchanja Yohana.

Naye kocha wa gym ya Mafia boxing Said amesema waliamua kuja na sparing hiyo ili kuwaandaa wachezaji wake na pambano la Knock out ya mama na kupitia hivyo amepata nafasi ya kuwaangalia mabondia wake kama mafunzo waliyoyapata yamewajengea uwezo mkubwa wa kupambana.

"Leo hii sparing mnayoiona hapa ni Kipimo ili Kuona ni nini ambacho mabondia wetu wamekipata katika mazoezi ambayo tuliwapatia hapo awali kule maeneo ya minaki,Kisarawe na nimeona kile tulichowafundisha wamekifanya Kazi kwa asilimia kubwa zaidi ya 99  na sehemu ya mapungufu pia tutairekebisha "alisema Kocha Said.

Hata hivyo kocha huyo alisisitiza kuwa jina la Knock out ya mama hajijaletwa kwa makusudi kwani watanzania sasa watajionea kwa mara ya kwanza maana halisi ya jina hilo katika pambano Kali la masumbwi la kimataifa hivyo wajitokeze kwa wingi kushuhudia siku ya pambano May 25,2025 katika viwanja vya Posta Kijitonyama.

Comments