Skip to main content

MAMLAKA YA HALI YA HEWA YATANGAZA MWELEKEO WA HALI YA HEWA KIPINDI CHA JUNI HADI AGOSTI 2025

 

MAMLAKA YA HALI YA HEWA  YATOA MWELEKEO WA HALI YA HEWA KIPINDI CHA JUNI HADI AGOSTI 2025


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Ladislaus Chang’a amesema kwa kawaida, kipindi hiki, hutawaliwa na hali ya baridi na upepo mkali kwa maeneo mengi ya nchi. 

NA MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa hali ya joto, upepo na mvua katika msimu wa Juni hadi Agosti (JJA), 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 22, 2025 jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Ladislaus Chang’a amesema kwa kawaida, kipindi hiki, hutawaliwa na hali ya baridi na upepo mkali kwa maeneo mengi ya nchi. 

Kuhusu mwelekeo wa hali ya joto Dkt. Chang'a amebainisha kuwa hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi ambapo hata hivyo, hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Singida pamoja na maeneo ya magharibi mwa mkoa wa Dodoma.

"Vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza katika mwezi Julai. Vipindi vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, ukanda wa mwambao wa pwani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba," amesema Dkt. Chang'a.

Kwa upande wa mwelekeo wa hali ya upepo amesema Msimu wa Kipupwe 2025 unatarajiwa kutawaliwa na upepo wa wastani utakaovuma kutoka Kusini Mashariki kwa maeneo mengi ya nchi, na vipindi vichache vya upepo mkali utakaovuma kutoka kusini (upepo wa kusi) hususan katika kipindi cha miezi ya Juni na Julai 2025 katika maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu.

Kwamba athari zake ni magonjwa yanayohusiana na hali ya hewa ya baridi kama vile homa ya mapafu na magonjwa ya mifugo yanaweza kujitokeza, ingawa kwa kiasi kidogo na kwamba hali ya vumbi linalosababishwa na upepo katika baadhi ya maeneo linaweza kupelekea uwepo wa magonjwa ya macho. 

Kuhusu matarajio ya viwango vya joto kwa kipindi hicho, Dkt. Chang'a amebainisha kwa katika kipindi cha msimu wa Kipupwe (JJA) 2025, hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. 

Hata hivyo, amesisitiza kuwa hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Singida pamoja na maeneo ya magharibi mwa mkoa wa Dodoma na kwamba vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza katika mwezi Julai. 


Amesema kwa Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu), hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10 oC na 18 oC.


Kwamba kwa Ukanda wa pwani ya kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi. 


Ameeleza, kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 16oC na 24oC kwa maeneo ya mwambao wa pwani na visiwani na kati ya nyuzi joto 12oC na 20oC katika maeneo ya nchi kavu ambapo hata hivyo, maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 12oC. 

Kwa upande wa Nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara), hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi na kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10 oC na 20 oC.

Hata hivyo, maeneo yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 10 oC huku Kanda ya magharibi (Mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma), hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10⁰C na 18⁰C. 

Dkt. Chang'a amebainisha, Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma), hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo mengi ya mkoa wa Singida na magharibi mwa mkoa wa Dodoma. 

Hata hivyo, hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo ya mashariki mwa mkoa wa Dodoma na kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10oC na 20oC huku Ukanda wa pwani ya kusini  (Mikoa ya Mtwara na Lindi), hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 12 oC na 20 oC.

Kwa Kanda ya kusini (Mkoa wa Ruvuma), hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 8oC na 16 oC.

Ameongeza kuwa Nyanda za juu kusini-magharibi (Mikoa ya Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro), hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi. Hata hivyo, hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo ya mkoa wa Rukwa. Kiwango cha joto la chini katika maeneo haya kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 6oC na 20oC. Aidha, maeneo yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 6 oC.

Akizungumzia kuhusu mwelekeo wa mvua kwa kipindi hiki, amesema kwa kawaida kipindi cha msimu wa Kipupwe (JJA) hutawaliwa na hali ya ukavu katika maeneo mengi ya nchi.

Hata hivyo kwa JJA 2025, vipindi vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria hususan Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu na Mara pamoja na ukanda wa pwani na maeneo ya nchi kavu (mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Mtwara, Lindi, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba).

Kuhusu mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa amesema katika msimu wa Juni hadi Agosti 2025, joto la bahari katika ukanda wa tropiki ya kati ya Bahari ya Pasifiki linatarajiwa kuwa la wastani. 

Kwamba kwa Bahari ya Hindi, joto la Bahari la juu ya wastani linatarajiwa katika maeneo ya mashariki (pwani ya Indonesia), wakati joto la bahari la wastani linatarajiwa katika maeneo ya magharibi mwa Bahari ya Hindi (pwani ya Afrika Mashariki). 

Kwamba hali hizi za bahari kwa pamoja zinatarajiwa kuwa na mchango hafifu katika mifumo ya hali ya hewa hapa nchini.

Kwa upande mwingine, joto la bahari katika eneo la kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi (kusini mwa Madagascar) linatarajiwa kuwa la juu ya wastani. Hali hii inatarajiwa kudhoofisha mgandamizo mkubwa wa hewa katika eneo hilo na hivyo kupunguza kasi ya upepo wenye baridi kutoka kusini kuelekea katika maeneo ya nchi yetu. 

Comments