MHE. ZAIDAT FUNDI ATOA WITO WA AMANI NA MAADILI YA KISIASA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

 MHE. ZAIDAT FUNDI ATOA WITO WA AMANI NA MAADILI YA KISIASA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU


Zanzibar,

Mwenyekiti wa Kigoda cha Wanawake Taifa wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Mhe. Zaidat Fundi, leo ametoa wito kwa Watanzania wote kulinda amani ya taifa na kujiepusha na aina yoyote ya uchochezi, hasa kupitia mitandao ya kijamii. Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho zilizopo Uwanja wa Ndege Zanzibar, Mhe. Zaidat alisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya kisiasa.


Akizungumzia hali ya sasa ya mijadala mitandaoni, Mhe. Zaidat alieleza kuwa kumekuwa na ongezeko la lugha za kejeli na kashfa dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jambo ambalo linakosa staha na utu. Alisisitiza kuwa:


> "Watanzania na Wanaafrika Mashariki wanapaswa kuelewa kuwa Rais wa Tanzania ni mwanamke. Kumkosoa mwanamke kunahitaji staha, utu, na nidhamu. Hatupingi kumkosoa Rais, lakini tujiulize, tunamkosoaje? Ukosoaji wa mitandaoni usiwe jukwaa la kumdhalilisha mtu mwenye hadhi ya mzazi wako. Hapana! Huo si utamaduni wetu, hatukuumbiwa hivyo wana Afrika Mashariki. Tunapaswa kujitathmini upya."




Kuhusu maandalizi ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, Mhe. Zaidat alitoa rai kwa vyombo vya usalama kuhakikisha vinachukua hatua stahiki kulinda usalama wa nchi. Alibainisha kuwa amani ni msingi wa maendeleo katika taifa lolote, hivyo vyombo vya usalama vinapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha hali hiyo inadumishwa.


Akipendekeza hatua za kuimarisha elimu ya kiraia, Mhe. Zaidat alitoa wito kwa Tume Huru ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama vya Siasa, na Jeshi la Polisi kuandaa makongamano ya kitaifa yatakayotoa elimu kwa wananchi kuhusu haki, mipaka, na majukumu yao wakati wa uchaguzi. Alisema:


> "Watanzania wanapaswa kupewa elimu ya madhara ya uchochezi wa mitandaoni na kuelewa uzito wa kesi zinazohusiana na uchochezi. Tunahitaji uchaguzi wa amani, unaozingatia sheria, maadili, na utu."




Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Zaidat alisisitiza kuwa uongozi bora hujengwa katika msingi wa maadili, nidhamu, uelewa wa elimu ya kiraia, na ushiriki wa haki katika mchakato wa kidemokrasia, hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Comments