Msando: Boda Boda Wasajiliwe Katika Vikundi vya Ushirika Ili Kukopesheka
Msando: Boda Boda Wasajiliwe Katika Vikundi vya Ushirika Ili Kukopesheka
Dar es Salaam, Mei 28, 2025 – Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Albert Msando, ametoa agizo kwa uongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha waendesha pikipiki maarufu kama boda boda wanasajiliwa katika vikundi rasmi vinavyoweza kujiunga na vyama vya ushirika, hatua itakayowawezesha kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali za kifedha nchini.
Mhe. Msando alitoa agizo hilo alipokuwa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika ufunguzi wa mkutano wa jukwaa la ushirika wa Mkoa huo, ambapo alisisitiza kuwa boda boda ni kundi muhimu katika kuchochea uchumi wa nchi endapo litapangwa ipasavyo kupitia mfumo wa ushirika.
"Waendesha boda boda wengi wanashindwa kukopesheka kwa sababu ya kukosa dhamana, lakini kupitia usajili katika vikundi vya ushirika, wataweza kuaminika zaidi na kupata mikopo ya maendeleo," alisema Msando.
Ameongeza kuwa madereva wengi wamekuwa wakinyonywa na wamiliki wa pikipiki kwa kupewa mikataba isiyo na tija, hivyo ushirika unaweza kuwa mkombozi kwao kiuchumi.
Katika kulitatua hilo, Msando aliliagiza baraza la usalama na viongozi wa kata kuhakikisha kila boda boda anakuwa na nyaraka muhimu ikiwemo cheti cha kuzaliwa, namba ya NIDA, leseni ya udereva na bima ili nyaraka hizo ziwasaidie kujiunga na vyama vya ushirika na kuanza kukopesheka.
"Ni jambo lisilokubalika dereva aliyelipa Shilingi 300,000 kwa mwezi kushindwa kumudu gharama za leseni na bima. Nitahakikisha kila dereva wa Wilaya yangu anapata sifa zinazostahili ili ajiunge na ushirika na kukopesheka na mimi kama mkuu wa Wilaya ya Ubungo nitalisimamia hili mwenyewe kwani wakati wa bodaboda kupewa mikataba ya kinyonyaji na wamiliki wa bodaboda hizo umefika ukingoni sasa,” alisisitiza.
Aidha, Msando alipongeza juhudi za vyama vya ushirika Mkoa wa Dar es Salaam kwa mchango wao katika ajenda za maendeleo kupitia sekta hiyo.
Katika hatua nyingine, alieleza kuwa Serikali kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeshatoa zaidi ya Shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuanzisha benki ya ushirika itakayowawezesha wanachama kupata huduma bora za kifedha.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Dar es Salaam, Enerest Nyambo, alisema kuwa jukwaa hili ni la nane kufanyika, na kwamba wana dhamira ya kutoa suluhu kwa waajiri na waajiriwa katika kutatua changamoto zinazojitokeza sehemu za kazi, ili kuhakikisha hakuna mtu anayepata dhuluma.
Alieleza kuwa wanapata ufadhili kutoka taasisi mbalimbali zinazojihusisha na utoaji wa mikopo katika maeneo tofauti, jambo ambalo limewezesha kuwa na jukwaa bora.
Aidha, mwenyekiti huyo aliongeza kuwa wamepokea maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ndugu Albert Chalamila.
"Vilevile, tumepokea maelekezo yote tuliyopewa, na tutaenda kuyatekeleza kwa wakati. Pia tunawasihi watu wote kutoka katika vyama vya ushirika nchini kufuata taratibu zote zinazohusiana na utoaji wa mikopo," alisema Mwenyekiti Nyambo.
Comments