Wakili Peter Madeleka anautaka Ubunge Jimbo la Kivule, ajitosa rasmi kutaka kuuwania
Wakili Peter Madeleka anautaka Ubunge Jimbo la Kivule, ajitosa rasmi kutaka kuuwania
Wakili maarufu hapa nchini ambaye siku chache zilizopota alitangaza kujiondoa rasmi ndani ya chama Cha demokrasia na maendeleo, Chadema na kujiunga na Act Wazalendo ajitosa rasmi kuwania Ubunge wa Jimbo la Kivule kupitia chama hicho.
Wakili Madeleka Leo Mei 31, amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama chake ili kuteuliwa kuwa mpeperusha bendera wa chama hicho katika nafasi ya Ubunge huku akisindikizwa na kulakiwa na mamia ya wanachama na viongozi.
Mara baada ya kuchukua fomu hiyo,wakili Madeleka ameahidi kuleta mabadiliko ya kweli kwa wananchi wa Kivule ambao amedai wamepitia kipindi kigumu Cha changamoto mbalimbali ikiwemo ubovu wa barabara ndani ya jimbo hilo jipya la Uchaguzi ambalo limegawanywa kutoka Jimbo la Ukonga ambalo Mbunge wake ni Jerry Slaa
"Wananchi wamechoka na hali ngumu ya maisha. Miundombinu ni mibovu, bei za bidhaa zipo juu, huduma za afya na elimu ni duni. Haya yote ni matokeo ya mfumo wa uongozi wa CCM. Lakini hatuwezi kususa ,hatuwezi kumuachia fisi bucha bali tunapaswa kushiriki, kupigania, na kushinda mabadiliko."amesema Madeleka.
Aidha wakili huyo amesema kuwa huu si wakati wa kulalamika pembeni, bali kushiriki kikamilifu kwenye uwanja wa demokrasia na si kususia kama kilivyofanya chama kingine cha upinzani.
Akijibu swali la waandishi wa habari ambao walitaka kufahamu kwa nini hajaenda kugombea ubunge kwao mkoani Tabora ambako ametokea na kuamua kugombea jimbo la Kivule,amesema kuwa ameamua kugombea katika jimbo hilo kwani Kuna changamoto lukuki kuliko Tabora.
"Kwa mujibu wa katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania,mtanzania yoyote anaweza kugombea popote ndani ya mipaka ya nchi na Tabora ni kwetu lakini nimeamua kutoa kipaumbele cha Kivule kwa sababu matatizo yake ni makubwa kuliko ya ninakotokea ambako sijawahi kugombea ubunge" amesisitiza.
Comments