ACT NI 'MAPIGO NA MWENDO' DAR,YAWATAKA WATANZANIA WAJITOKEZE KUPIGA KURA,yasema watalinda kura zao
ACT NI 'MAPIGO NA MWENDO' DAR,YAWATAKA WATANZANIA WAJITOKEZE KUPIGA KURA,yasema watalinda kura zao
NA MWANDISHI WETU
CHAMA cha ACT Wazalendo kimeendelea na mikutano ya hadhara katika Mkoa wa Dar es Salaam kuinadi operesheni Linda Demokrasia kupitia kampeni ya 'Oktoba Linda Kura' yenye lengo kuhamasisha wananchi kuhakikisha wanalinda kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba Mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika leo Juni 18, 2025 kwenye Viwanja vya Bakhresa, Manzese mkoani humo, Katibu Mkuu wa Chama hicho Ado Shaibu amesema watahakikisha operesheni hiyo wanaifikisha kila Jimbo la Mkoa huo.
Shaibu amesema mwizi wa kura ni kama mwizi anayevunja duka, kuiba fedha na kufanya matukio mengine kama hayo hivyo anapaswa kushughulikiwa kama wezi wengine.
Kwa upande wake Kada wa Chama hicho, Sheikh Ponda Issa Ponda, amesisitiza katika uchaguzi ujao, chama hicho kitaongoza mapambano ya kulinda kura za wananchi.
Amesema ni muhimu kupambana ndani ya eneo la vita kuliko nje ya uwanja wa mapambano, na kwamba hiyo ndiyo njia pekee ya kukiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ponda ambaye anafahamika kwa misimamo yake ya kupigania haki za binadamu, amesema inawezekana kushinda uchaguzi ujao kwa kutumia nguvu ya wananchi kama ilivyokuwa mwaka 2010 ambapo wapinzani wengi walishinda kwa kutumia nguvu hiyo hiyo ya umma.
"Wale Polisi ni binadamu kama tulivyo sisi, inakuwaje ifike mahala ushindwe kuelewana naye? Ni binadamu mwenzako, tutatumia lugha zinazoweza kueleweka, kila mahala kuna lugha yake," amesema Ponda huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
Amesema kwa kufanya hivyo wataweza kujenga ujasiri kwa wananchi kupambana na kutetea haki zao.
Ponda amesema hakuna sababu ya kuendelea kuwa na utawala ambao unatoza gharama kubwa kwa wafu, huku akitolea mfano wagonjwa wa figo ambao wanalazimika kutumia Shilingi 540,000 kila wiki kwa ajili ya matibabu, na endapo hawatapata fedha hizo wanakabiliwa na kifo.
"Hakuna serikali kama mtu anaweza kuchukuliwa akauawa, na waliofanya kitendo hicho wasijulikane. Tuna sababu gani ya kuendelea kuwa na serikali ya namna hii?" amehoji Ponda.
Naye Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa Chama hicho Abdul Nondo amesema wananchi ndio wenye mamlaka ya kuiwajibisha serikali hivyo wana kila sababu ya kuwa imara na kuiwajibisha serikali kupitia wawakilishi ambao wanaweza kuwachagua kwenye uchaguzi mkuu.
Nondo amewataka wananchi kufahamu nafasi yao kuiwajibisha serikali hivyo wasikubali kushawishiwa kutokupiga kura.
Pamoja na hayo Nondo amewaita wale wanaohamasisha watu kutokupiga kura na kususia uchaguzi kuwa ni 'wanyonge' na wamekubali kuwa wanyonge.
Kadhalika Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo Bara, Esther Thomas ametoa wito kwa Watanzania kutokuacha kushiriki uchaguzi na kupiga kura kwani maendeleo ya nchi yanaamuliwa kwa kuchagua viongozi wanaofaa kwenda kuwawakilisha wananchi na baada kupigiwa kura.
- Get link
- X
- Other Apps
Comments