CHAUMMA CHAWAITA WAGOMBEA FOMU KWA WAGOMBEA WA UBUNGE NA UDIWANI KUANZIA KUTOLEWA LEO

 CHAUMMA CHAWAITA WAGOMBEA  FOMU KWA WAGOMBEA WA UBUNGE NA UDIWANI KUANZIA KUTOLEWA  LEO

Dar es Salaam — Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimepuliza kipenga rasmi kwa mwanzo wa mchakato wa kugombea nafasi za ubunge na udiwani kupitia chama hicho, huku nafasi ya urais ikiwekwa kiporo kwa sasa.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa CHAUMMA, Salum Mwalimu, ametangaza kuwa kuanzia leo, Julai 1, 2025, milango itakuwa wazi kwa wanachama na wananchi wote wenye sifa na nia ya kugombea nafasi za udiwani na ubunge kuchukua fomu za maombi kupitia chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

"Ni wakati sahihi kwa wanachama wetu na hata wale ambao bado si wanachama, lakini wana dhamira ya kugombea kupitia CHAUMMA, kujiandaa kuchukua na kujaza fomu kwa kufuata utaratibu uliowekwa na chama," alisema Salum Mwalimu.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, waombaji wote wa nafasi za ubunge na udiwani (vikiwemo viti maalumu) kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, watalazimika kuonyesha nia ya kugombea katika maeneo husika kabla ya kupewa fomu rasmi. Hii ni hatua ya awali ya kuonesha dhamira ya kweli ya kugombea na kutambua uhusiano wa mgombea na jamii anayotaka kuiwakilisha.

Uamuzi huu wa CHAUMMA unakuja siku chache baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutangaza ratiba yake ya kuchukua na kurejesha fomu kwa wagombea wake wa ubunge, udiwani na uwakilishi, ambayo inaendelea kuanzia Juni 28 hadi Julai 2, 2025.

Kwa sasa, nafasi ya kugombea urais kupitia CHAUMMA bado haijatangazwa rasmi, huku chama kikieleza kuwa suala hilo litafuatia baada ya hatua ya awali ya kupokea wagombea wa ngazi nyingine kukamilika.

Chama hicho kimehimiza utulivu, uwazi na uzingatiaji wa kanuni za chama katika mchakato mzima wa kuchukua na kurejesha fomu, kikisema kuwa kinadhamiria kutoa nafasi sawa kwa kila mwanachama mwenye sifa. 

Comments