TLP haitoi Vyeo kwa Wageni wanaohamia bila baraka za Wanachama:Lyimo

 

TLP haitoi Vyeo kwa Wageni wanaohamia bila Baraka za Wanachama:Lyimo




Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) kimetangaza msimamo wake dhidi ya utaratibu wa baadhi ya vyama vya siasa kuwapa madaraka viongozi wapya wanaohamia kutoka vyama vingine, kikisisitiza kuwa hakitatoa nyadhifa kwa wageni bila ridhaa ya wanachama.

Akizungumza jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari waliomtembelea ofisini kwake, Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Bw. Lyimo, alisema TLP kimejengwa juu ya misingi ya kuheshimu wanachama wake na kinaamini uwezo wa viongozi waliopo kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Hakuna nyadhifa ambayo mtu anaweza kuja tu hapa tukampa. Lazima vikao vikae, viangalie uwezo wa aliyepo kabla ya kuamua kumpa mwingine. Kwa sasa, uongozi uliopo makao makuu una uwezo wa kutosha,” alisema Lyimo.

Madaraka kwa Wageni Yasababisha Madhara

Bw. Lyimo alieleza kuwa uzoefu wa huko nyuma unaonesha madhara ya kutoa madaraka kwa wageni bila kufuata utaratibu. Alitoa mfano wa kijana mmoja aliyeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Vijana pasipo kujua Katiba ya chama, ambaye baadaye aliitisha mkutano mkuu kinyume na taratibu.

“Huyu kijana alikuja tu akapewa nafasi kubwa. Baadaye akaanza kufanya maamuzi makubwa bila kuelewa mfumo wa chama, na hata kuniandikia barua mimi kama Katibu Mkuu wakati ule, ananitaka nihudhurie mkutano wake batili,” alieleza kwa ukali.

Usawa wa Kijinsia wapewa Kipaumbele

Katika hatua nyingine, TLP imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha usawa wa kijinsia katika uongozi wa chama. Bw. Lyimo alisema chama hicho kinatetea mfumo wa hamsini kwa hamsini, ambapo wanawake wanapewa nafasi sawa na wanaume katika ngazi zote za maamuzi.

“Hatuimbi wimbo wa Samia, ila tunaimba wimbo wa ushirikishwaji. Mama Samia ni mfano wa uongozi thabiti wa mwanamke. Tunataka wanawake wetu wapate nafasi, wajifunze na wachangie maendeleo ya Taifa,” alisema.

Mchakato wa Uchaguzi wa Ndani Unaendelea

TLP pia imetangaza kuwa linaendelea na zoezi la utoaji wa fomu kwa watia nia wa Ubunge na Udiwani, ambalo lilianza Mei na linatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu. Baada ya hapo, chama kitatoa taarifa rasmi kabla ya kuanza mchujo wa kuwapata wagombea bora wa kupeperusha bendera ya chama hicho.

Comments