Masoud Maftah Aahidi Kuendelea Kuwa Mwanachama Mtiifu wa CCM Licha ya Jina Kutorudi Katika Mchujo

 Masoud Maftah Aahidi Kuendelea Kuwa Mwanachama Mtiifu wa CCM Licha ya Jina Kutorudi Katika Mchujo

Dar es salaam

Siku moja mara baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, kutangaza majina ya wagombea walioteuliwa kuendelea katika mchakato wa kura za maoni ili kumpata mgombea mmoja wa nafasi ya Ubunge kwa kila Jimbo hapa nchini, aliyekuwa mmoja wa watia nia waliochukua fomu kuomba ridhaa ya chama hicho Jimbo la Kinondoni, Masoud Maftah, amesema kuwa ataendelea kuwa mwanachama mtiifu kwa chama hicho licha ya jina lake kutorudi.

Maftah ameyasema hayo leo Julai 30, 2025, kwenye mahojiano maalum na waandishi wa habari waliotaka kupata maoni yake baada ya orodha ya majina ya wagombea kutajwa, huku akiongeza kuwa atamuunga mkono mgombea yoyote ambaye wajumbe wa chama hicho watampitisha kwenye kura za maoni.

"Unajua kwenye kila mchakato lazima kuna ambao watashinda na ambao hawatashinda. Hata katika mbio za magari kuna mshindi, na kwenye chama changu kulikuwa na wagombea wengi na chama kimefanya kazi kubwa kuwapata ambao wataendelea na hatua inayofuata," amesema.

Aidha, ameongeza kuwa atapita kila mtaa na kila eneo katika Wilaya ya Kinondoni akiwa bega kwa bega kumnadi mgombea yoyote ambaye atapitishwa na chama hicho.

"Mimi nitaendelea kuwa mtiifu kwa chama na viongozi wangu wote, na siwezi kuondoka kwenye chama kwani naamini wakati wa Mungu ni wakati sahihi, na nitapita kila uchochoro kukitafutia Chama Cha Mapinduzi kura na kuhakikisha kinashinda kwa kishindo," amesema.

Walioteuliwa kuendelea katika hatua ya kura za maoni ni pamoja na Mbunge anayemaliza muda wake, Abas Tarimba, Bi Jerusa Kitoto atachuana na wengine saba akiwemo Iddi Azan, Wilfred Elias Nyamwija, Michael Richard Wambura, Adv. Julieth Venant Rushuli, Wangota Mussa Salum na Zena Khalfani Kiputiputi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Chama Cha Mapinduzi, sasa watia nia wote waliogombea ridhaa ya kuteuliwa kuwania nafasi za Ubunge ambao wamepitishwa na Kamati ya Halmashauri Kuu ya chama hicho, sasa watakwenda kujitambulisha kwa wajumbe na kisha baadaye kushiriki katika mchakato wa kupigiwa kura za maoni

Comments