Skip to main content

OFISI YA MKEMIA MKUU YAWEKA WAZI, UWEKEZAJI MKUBWA WA MITAMBO NA VIFAA VYA KISASA ULIOFANYWA NA SERIKALI, lengo kuboresha huduma za uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara nchini.

 

OFISI YA MKEMIA MKUU YAWEKA WAZI, UWEKEZAJI MKUBWA WA MITAMBO NA VIFAA VYA KISASA ULIOFANYWA NA SERIKALI, lengo kuboresha huduma za uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara nchini.



Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (MMS), Dkt. Fidelice Mafumiko akiwasilisha mada kwa wahariri wa vyombo vya habari katika kikaokazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kilichofanyika Kwenye hoteli ya King Jada jijini Dar es Salaam. 


NA MWANDISHI WETU 

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Mabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (MMS), Dkt. Fidelice Mafumiko amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefanya uwekezaji mkubwa katika mitambo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuboresha huduma za uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara nchini.

Dkt. Mafumiko amebainisha hayo leo Julai 10, 2025 jijini Dar es Salaam akieleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha Miaka Minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Utawala wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kikao cha Wahariri na Waandishi wa habari kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

"Uwekezaji huu umewezesha ongezeko la thamani ya mitambo kutoka Shilingi Bilioni 13.6 mwaka wa fedha 2017/2018 hadi Shilingi Bilioni 17.8 mwaka wa fedha 2024/2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 23.6. Kiasi hicho kimetumika kununua mitambo mikubwa 16 na midogo 274, hatua iliyosaidia kuboresha ufanisi wa uchunguzi wa kimaabara kwa wananchi," amesema Dkt. Mafumiko.

Kuhusu ubora wa huduma zinazotolewa na Mamlaka hiyo, Dkt. Mafumiko ameeleza kuwa Mamlaka imefanikiwa kutoa huduma za uchunguzi wa kimaabara zinazokubalika kitaifa na kimataifa kwa kutekeleza mifumo ya ubora na umahiri yenye viwango vya kimataifa kama ISO 9001:2015 na ISO 17025:2017.

Kwamba katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mamlaka imefanikiwa kupata ithibati ya mfumo wa umahiri wa uchunguzi wa kimaabara (ISO 17025:2017) katika maabara sita ambazo ni, Maabara ya Vinasaba vya Binadamu, Mikrobiolojia, Sayansi Jinai, Toksikolojia, Mazingira Maabara ya Chakula na Kanda ya Ziwa – Mwanza.

Kwa upande wa udhibiti wa kemikali, Dkt. Mafumiko amesema Mamlaka inatekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani Na. 3 ya mwaka 2003 ambapo Sheria hiyo inalenga kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya athari za kemikali.

Akibainisha mafanikio katika kipindi cha miaka minne ya Rais Dkt. Samia amesema kwenye usajili wa wadau, ni kwmaba idadi ya wadau waliosajiliwa imeongezeka kutoka 2,125 mwaka 2021 hadi kufikia 3,835 Juni 2025, ongezeko la asilimia 81.

Kadhalika kuhusu, ukaguzi wa Maghala, Mamlaka imekagua maghala 8,521 ya kuhifadhia kemikali, ikiwa ni asilimia 119 ya lengo la ukaguzi wa maghala 7,160, wakati kuhusu Vibali vya Kuingiza/Kusafirisha Kemikali ni kwamba vibali vya kuingiza kemikali vimeongezeka kutoka 40,270 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 67,200 mwaka wa fedha 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 40.

Kwamba Mamlaka pia imechangia uboreshaji wa mazingira ya biashara ya kemikali nchini, hasa zile zinazotumika katika sekta ya madini. Dkt. Mafumiko alieleza kuwa matumizi ya kemikali muhimu yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka minne.




Comments