Sigrada Mligo Ajiuzulu CHADEMA, Alalamikia Unyanyasaji wa Ndani na Kubezwa kwa Mchango Wake,Atimkia Chaumma
Sigrada Mligo Ajiuzulu CHADEMA, Alalamikia Unyanyasaji wa Ndani na Kubezwa kwa Mchango Wake
Dar es Salaam, Tanzania — Aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA), Sigrada Mligo, ametangaza kujiondoa rasmi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akilalamikia kile alichokitaja kuwa ni unyanyasaji wa ndani ya chama na kubezwa kwa mchango wake wa muda mrefu.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu hii katika makao makuu ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), yaliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, Mligo amesema hatua yake imesababishwa na maumivu aliyoyapata kutokana na kuhusishwa na migogoro ndani ya CHADEMA, licha ya mchango mkubwa alioutoa hasa wakati wa nyakati ngumu za kisiasa.
“Mwaka 2019 tuliendesha kampeni ya CHADEMA Digital kwa ajili ya usajili wa wanachama na maandalizi ya uchaguzi. Lakini katika uchaguzi wa Januari 2025, chama kilishindwa kufanya operesheni katika majimbo ya Makete, Wang’ing’ombe na Ludewa kwa sababu ya ukosefu wa bajeti,” alisema Mligo.
Kwa mujibu wa Mligo, hali hiyo ilimlazimu kutumia fedha zake binafsi—zaidi ya shilingi milioni 15—kufanikisha operesheni hiyo ili kuhakikisha majimbo hayo matatu kutoka Mkoa wa Njombe yanashiriki kikamilifu uchaguzi wa ndani ya chama.
“Niligharamia shughuli zote hadi majimbo hayo yakapata viongozi waliohusika kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa chama. Yote yako kwenye kumbukumbu rasmi, hawawezi kuyakana,” alisisitiza.
Hata hivyo, licha ya kujitolea kwake, Mligo anadai kuwa baadhi ya wanachama na viongozi wa CHADEMA wamekuwa wakimdharau na kumpachika majina ya kubeza, wakimhusisha na madai ya kuhujumu chama.
“Kuna watu wanatumia lugha za kubeza wakijiona ndio waliokifia chama. Mimi si mtu wa matangazo wala mitandaoni, lakini ukweli ni kuwa nimefanya mengi kwa ajili ya CHADEMA. Inasikitisha mtu kusema kuwa Sigrada anakiua chama, hali ya kuwa nimetoa sadaka yangu ya hali na mali kwa chama hiki,” alisema kwa masikitiko.
Hata hivyo Bi Mligo ameongeza kuwa tangu alipopigwa na msaidizi Makamo Mwenyekiti wa Chadema bara, John Heche na baadaye kulazwa hospitali na kutembelewa na baadhi ya wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa ikiwemo chama Cha Mapinduzi CCM ambao pia walimlipia fedha za matibabu pamoja na gari la kubeba wagonjwa 'Ambulance' waliibuka vijana wa chama hicho wakimtupia lugha za matusi mitandaoni kwa kusema kuwa anataka kukiua chama hicho hivyo ameamua kujiondoa ili chama hicho kife bila uwepo wake.



Comments