TANESCO YAGAWA MAJIKO YA UMEME SABASABA, YATOA ELIMU YA NISHATI SAFI KWA WATU WENGI

 

TANESCO YAGAWA MAJIKO YA UMEME SABASABA, YATOA ELIMU YA NISHATI SAFI KWA WATU WENGI




NA MWANDISHI WETU 

Katika kilele cha shamrashamra za Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewasha moto wa matumaini kwa wananchi – si kwa maneno, bali kwa vitendo ambapo Leo, Julai 7, 2025, mamia ya wananchi waliojipanga kwenye banda la TANESCO wameondoka na zawadi ya majiko ya umeme, hatua iliyowavutia wananchi wengi kutembelea banda hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, alizungumza na waandishi wa habari huku akielezea dhamira ya shirika hilo kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

 “Ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwa sasa ni wakati wa mabadiliko. Tunahama kutoka kwenye kuni na mkaa – sasa ni zamu ya umeme kusafisha hewa yetu na kulinda afya zetu,” alisisitiza.

Lakini si kila mtu alipata zawadi kirahisi,bali Wananchi walilazimika kupambana katika mashindano ya kujibu maswali kuhusu nishati safi. 

Washindi waliibuka na majiko haya maalum ya umeme – ambayo yana uwezo wa kupika chakula kwa chini ya Unit moja tu! Ndiyo, chini ya Unit moja – mapinduzi ya kweli jikoni


Kwa upande mwingine, kampuni tanzu ya TANESCO, ETDCO, nayo haikubaki nyuma. Sadock Mugendi, Kaimu Meneja Mkuu, alifichua mafanikio ya kusisimua ya kumaliza mradi wa kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Katavi – umbali wa km 383 – kwa msongo wa 132kV Na si hivyo tu, miradi zaidi inatekelezwa Mbeya na maeneo mengine vijijini, ikilenga kulifikisha umeme hadi pembezoni kabisa mwa nchi.

Na kama hiyo haitoshi – habari mpya kutoka TGDC, kampuni ya uendelezaji wa nishati ya joto ardhi, zinasisimua zaidi! Mathew Mwangomba, Meneja Mkuu, amethibitisha kuwa eneo la Mbozi, Mbeya, limebainika kuwa na uwezo wa kuzalisha hadi megawati 70 za umeme safi wa jotoardhi, ambao utachangia moja kwa moja kwenye Gridi ya Taifa.



Nishati safi sio ndoto tena – ni sasa!

TANESCO na washirika wake wanaandika historia, huku wakitoa fursa kwa Watanzania sio tu kupata elimu bali pia vifaa vya kuwasha maisha mapya. Majiko yametolewa. Miradi inasonga. Na ndoto ya taifa lenye nishati safi inazidi kuwaka moto!

Comments