UVCCM Yazindua Mfumo wa Kisasa wa Kidijitali "Kijani Ilani Chatbot",vijana kuutikisa uzinduzi wa kampeni Dar

 

UVCCM Yazindua Mfumo wa Kisasa wa Kidijitali "Kijani Ilani Chatbot",vijana kuutikisa uzinduzi wa kampeni Dar





Dar es Salaam – Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa imezindua mfumo mpya wa kidijitali ujulikanao kama “Kijani Ilani Chatbot”, mfumo wa kisasa wa akili mnemba (AI) unaolenga kuchambua Ilani ya CCM na kutoa taarifa zote muhimu za maendeleo yaliyotekelezwa na chama hicho nchini.

Uzinduzi huo umefanyika leo katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, ukiongozwa na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohammed Ali Kawaida.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kawaida alisema mfumo huo utamwezesha kila mtumiaji kupata taarifa sahihi na majibu ya papo kwa papo kuhusu Ilani ya CCM, kulingana na mazingira ya eneo husika.

“Nawaomba vijana waitumie program hii kuondoa na kupinga taarifa za upotoshaji. Mfumo huu unatoa majibu yote muhimu kuhusu miradi iliyotekelezwa na itakayotekelezwa na chama chetu kote nchini,” alisema Kawaida.

Kuelekea Kampeni za CCM

Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa kuelekea uzinduzi wa kampeni za CCM Agosti 28, 2025 katika Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe – jijini Dar es Salaam, vijana wa UVCCM watafanya matembezi maalum ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki uchaguzi mkuu.

Aidha, aliwasihi vijana wa chama hicho waliogombea nafasi mbalimbali ndani ya CCM lakini majina yao hayakupita kutambua kuwa mchakato wa ndani ya chama umekwisha.

“Tusibaki na makundi. Tuwaunge mkono wagombea waliopitishwa, kwa sababu sisi sote ni kitu kimoja,” alisisitiza.

Katibu Mkuu UVCCM: Ni Mapinduzi ya Kidijitali

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Khalid Mwinyi, alisema mfumo wa Kijani Ilani Chatbot utakuwa chachu kubwa ya kukuza matumizi ya teknolojia nchini.

“Mfumo huu ni mapinduzi makubwa ya kidijitali. Vijana sasa mna nafasi ya kuuliza maswali yoyote na kupata majibu ya haraka kupitia teknolojia hii. Hii ni hatua kubwa ya maendeleo,” alisema.

Mwinyi pia alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa imani kubwa aliyoonesha kwa kumteua kuwa Katibu Mkuu wa UVCCM. Hata hivyo, alimpongeza pia aliyekuwa Katibu Mkuu wa UVCCM, Jokate Urban Mwengelo, kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya jumuiya hiyo.

Comments