WAZALISHAJI MAUDHUI MTANDAONI WATAKIWA KUCHAPISHA TAARIFA SAHIHI ZA UCHAGUZI MKUU
WAZALISHAJI MAUDHUI MTANDAONI WATAKIWA KUCHAPISHA TAARIFA SAHIHI ZA UCHAGUZI MKUU
NA MWANDISHI WETU
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, ametoa wito kwa wazalishaji wa maudhui mtandaoni kuhakikisha wanachapisha taarifa sahihi zisizo na upotoshaji ili kulinda amani na utulivu wa nchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Akizungumza leo Agosti 3, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kitaifa kati ya Tume na wazalishaji wa maudhui ya mtandaoni, Jaji Mwambegele alisisitiza kuwa matumizi mabaya ya teknolojia, ikiwemo akili bandia (AI), yanaweza kutumika vibaya na watu wenye nia ovu kusambaza taarifa za uongo na kupotosha umma.
"Nawasisitiza na kuwakumbusha umuhimu wa kuepuka matumizi mabaya ya akili bandia ambayo inatumiwa na baadhi ya watu kusambaza habari potofu kupitia mitandao ya kijamii," alisema Jaji Mwambegele.
Alieleza kuwa Tume ina imani kubwa na vyombo vya habari katika kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa mafanikio kutokana na ushirikiano wao wa awali katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, pamoja na ushiriki wao katika mikutano mbalimbali ya Tume.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhan Kailima aliwasihi wanahabari na wazalishaji wa maudhui kutumia kalamu na nyenzo zao kusambaza ujumbe wa amani katika kipindi chote cha uchaguzi.
"Tunawaomba kutumia fursa mlizonazo kuhakikisha kunakuwepo taarifa za mara kwa mara kuhusu kinachoendelea katika mchakato wa uchaguzi," alisema Kailima.
Aidha, alieleza kuwa vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee kuwa sauti ya kwanza kufichua upotoshaji wowote unaolenga kuharibu taswira ya Tume au kuathiri mchakato wa uchaguzi.
"Tume imejiwekea utaratibu wa kushirikiana kwa karibu na vyombo vya habari ili kuhakikisha uwazi na ushiriki wa wadau wote katika mchakato huu," aliongeza Kailima.
- Get link
- X
- Other Apps







Comments