KAMPENI ZA DKT SAMIA SULUHU HASSAN ZAWASHA MOTO: HIZI HAPA AHADI ZA SIKU 100 KWA WATANZANIA ZINAZOGUSA AFYA, ELIMU NA UJASIRIAMALI

 KAMPENI ZA DKT SAMIA SULUHU HASSAN ZAWASHA MOTO: HIZI HAPA AHADI ZA SIKU 100 KWA WATANZANIA ZINAZOGUSA AFYA, ELIMU NA UJASIRIAMALI


AHADI ZA SIKU 100 ZA DKT SAMIA SULUHU HASSAN.

Dkt Samia atatoa matibabu bila malipo kwa magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kwa wasiojiweza.

Katika ahadi zake ndani ya siku 100, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, imependekeza mpango wa kugharamia kwa asilimia 100 matibabu na vipimo vya kibingwa kwa wananchi wa kipato cha chini. Mpango huu unalenga magonjwa yasiyoambukizwa yenye gharama kubwa kama vile saratani, figo, moyo, kisukari, mifupa na mishipa ya fahamu ambayo yamekuwa kikwazo kwa wananchi wengi kumudu huduma za matibabu.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2025, Tanzania inakadiriwa kuwa na jumla ya watu milioni 65, ambapo takriban asilimia 26.4 ya wananchi hao sawa na watu milioni 17.16 wanatajwa na Benki ya Dunia kuwa wanaishi chini ya kiwango cha umasikini wa kipato. Hawa ndio wananchi wanaolengwa moja kwa moja na Rais Samia kupitia mpango huu wa huduma za afya bila malipo, kama sehemu ya ajenda ya kuimarisha usawa wa kijamii na haki ya msingi ya kupata matibabu kwa kila Mtanzania.


Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Coverage).

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, kila dola 1 inayowekezwa kwenye bima ya afya huleta faida ya hadi dola 5 kwa uchumi kupitia kuongezeka kwa tija ya kazi, kupungua kwa siku za kazi zilizopotea (utoro kazini).

Katika kutekeleza ahadi za siku 100 ya kuanzisha rasmi Mfumo wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote, Serikali inalenga kuwahudumia makundi maalum yenye uhitaji mkubwa wa huduma za afya wazee, watoto, mama wajawazito na watu wenye ulemavu ambao kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 wanachangia sehemu kubwa ya Watanzania milioni 61.7. Takriban asilimia 65.1 ya Watanzania hao wanaishi vijijini ambako huduma za afya ni changamoto.

Takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia 7 tu ya Watanzania waliokuwa na bima ya afya kufikia mwaka huo, hali inayodhihirisha pengo kubwa la upatikanaji wa huduma bora.

Ajira Mpya 5,000 Sekta ya Afya ndani ya siku 100 zitaisogeza Tanzania kutoka 92.6% hadi 95.2% ya lengo la WHO.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia mpango wa siku 100 wa Rais Samia Suluhu Hassan, imeahidi kuajiri wahudumu wa afya wapya 5,000, wakiwemo wauguzi na wakunga, ili kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto, kupunguza mzigo wa kazi kwa wahudumu waliopo, na kusaidia kaya maskini zenye wastani wa watu 4.3 kwa kaya.

Ajira hizi ni sehemu ya juhudi za kitaifa za kuimarisha mifumo ya afya na kufikia huduma jumuishi kwa wote. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2025, Tanzania ina jumla ya wahudumu wa afya wapatao 137,000, na uwiano wa mtoa huduma kwa wagonjwa ni 1:474, ikimaanisha kila mhudumu mmoja anahudumia watu 474. Ongezeko la ajira hizi litaongeza idadi ya wahudumu hadi takriban 142,000, na kuboresha uwiano huo hadi 1:458.

Kwa kuzingatia viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO), uwiano unaopendekezwa ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za msingi ni 1:439. Hii ina maana kuwa kila mhudumu mmoja anapaswa kuhudumia watu wasiozidi 439. Kwa mantiki hiyo, ongezeko la ajira hizi linaisogeza Tanzania kutoka asilimia 92.6 ya lengo la WHO hadi takriban asilimia 95.2.


Dkt Samia kutoa Bil 200 kwa biashara ndogondogo.

Kwa mujibu wa ILO na mashirika washirika kama AU, UNDP na Briter Bridges, sera za kuendeleza wafanyabiashara wadogowadogo kusini mwa Jangwa la Sahara zinalenga kuzalishasha ajira kwa vijana, ambapo asilimia 71.7 ya vijana wenye umri wa miaka kati ya 25–29 wanafanya kazi zisizo rasmi.

ILO inapendekeza serikali zitenge kati ya dola 10,000 hadi 100,000 kama ruzuku (sawa na shilingi milioni 25–250) sambamba na kuanzisha vituo vya ubunifu na miundombinu ya kidigitali. Mpango wa Tanzania wa kutenga shilingi bilioni 200 unalingana na viwango vya chini vya mitaji ya awali vinavyotambuliwa na ILO, na kuiweka nchi katika nafasi ya juu kikanda kwa uwekezaji wa moja kwa moja kwa sekta ya ujasiriamali, fedha hii inaweza kuanzisha biashara mpya 400,000 kwa mtaji wa awali wa shilingi 500,000.


Ajira za Walimu 7,000 wa Sayansi ndani ya siku 100 za Rais Samia ni ishara ya Uelekeo wa Tanzania ya Kidijitali.

Tanzania ina jumla ya wanafunzi 15,881,000 kuanzia awali hadi kidato cha sita, wakiwemo 1,567,000 wa awali, 11,200,000 wa msingi, 2,900,000 wa sekondari, na 214,000 wa kidato cha tano na sita.

Kati ya mwaka 2020 hadi 2024, ongezeko la wanafunzi limefikia 21.9% kwa awali, 14.9% darasa la kwanza, 46.2% kidato cha kwanza, na 62.0% kidato cha tano, likichochewa na utekelezaji wa elimu bila malipo.

Uwiano wa walimu kwa wanafunzi kwa sasa ni 1:163 kwa awali, 1:49 kwa msingi, na 1:27 kwa sekondari, ni juu ya viwango vilivyowekwa na UNESCO vya 1:25 kwa awali, 1:40 kwa msingi, na 1:25 kwa sekondari.

Kwa kutumia walimu wote wa sekondari waliopo nchini takriban 180,325 uwiano halisi wa sekondari unakuwa 1:16, ambao utazidi lengo la UNESCO kwa asilimia 35.6.

Ajira hizi za walimu wa sayansi na hisabati, ni sehemu ya ahadi za siku 100 za Rais Samia, inaonesha mafanikio ya kisera katika sekta ya Elimu.


Comments