Skip to main content

ZIMAMOTO WAANZA MAFUNZO YA UTAYARI WA UOKOAJI MAJINI,WASISITIZA WAKO VIZURI

 

 ZIMAMOTO WAANZA MAFUNZO YA UTAYARI WA UOKOAJI MAJINI,WASISITIZA WAKO VIZURI








Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wameanza mafunzo maalum ya uokozi katika maji kwa askari wake zaidi ya 20, yaliyoandaliwa na Tanzania Beach Lifeguards Organization yakifanyika kwenye bwawa la kuogelea la Shule ya Sekondari Shaaban Robert, Upanga jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 25, 2025 Msimamizi wa Mafunzo hayo kutoka Jeshi la Zimamoto Ilala Inspector Shani Juma amesema mafunzo hayo ni ya siku tatu ambapo yameanza leo Septemba 25, 2025 na yanatarajiwa kukamilika Septemba 27, 2025.

Inspector Shani amesema kuwa mafunzo hayo ni chachu ya kuongeza uwezo na kuimarisha utayari wa askari katika kukabiliana na majanga yanayohusiana na maji.

"Zimamoto na Uokoaji kazi yetu kubwa ni kuokoa. Huwezi kuokoa bila kujua, na huwezi kujua bila kufanya mazoezi. Kwa hiyo, tupo hapa kuongeza uwezo na kujiweka tayari kukabiliana na majanga ambayo yanaweza kutokea," amesema Inspector Shani.

Ameongeza kuwa mara nyingi askari wa uokoaji hufanya mazoezi baharini, hivyo kufanya mafunzo haya katika bwawa la kuogelea ni motisha na njia bora ya kujifunza mbinu sahihi zaidi za uokoaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tanzania Life Saving Society na kocha wa mafunzo hayo, John Belela, alisema lengo kuu ni kuwaweka tayari askari wa zimamoto na uokoaji ili waweze kushughulikia majanga kwa weledi.

"Tunapata matatizo kwenye maji. Vyombo vyetu vya usafiri wa majini vinaweza kupata shida. Mliona hata tukio la Zanzibar, ambapo meli ilizama na waokoaji walipofika walikuta tayari watu wengi wamefariki dunia. Kwa hiyo, mafunzo haya yatawajenga kuwa tayari wakati wote," amesema Belela.

Aidha, amebainisha kuwa programu hiyo itakuwa endelevu na imelenga kufika katika mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya kuwaongezea uwezo askari wa zimamoto na uokoaji.

Mafunzo hayo yameelezwa kuwa sehemu ya mkakati wa kuhakikisha Tanzania inakuwa na kikosi cha uokoaji chenye utayari wa hali ya juu kukabiliana na majanga yoyote yatakayojitokeza majini.

Comments