Kuje Ngombale Mwiru: Nikipata Ridhaa Nitaboresha Elimu, Afya na Ajira za Vijana

 

Kuje Ngombale Mwiru: Nikipata Ridhaa Nitaboresha Elimu, Afya na Ajira za Vijana



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Kuje Ngombale Mwiru, amesema kuwa ana matumaini makubwa ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu ujao, akiahidi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania mara tu atakapopewa ridhaa kupitia sanduku la kura.

Akizungumza leo Oktoba 9, 2025, katika makao makuu ya chama hicho yaliyopo Temeke, Jijini Dar es Salaam, Ngombale Mwiru alisema kampeni zake zimekuwa na mafanikio makubwa, huku akibainisha kuwa amepata fursa ya kukutana na wananchi katika maeneo mbalimbali na kusikia changamoto zao.

Amesema ameshazunguka katika mikoa ya Morogoro, Lindi, Mtwara, Mbeya na Iringa, na ziara hiyo itaendelea katika Tabora na hatimaye mikoa mingine yote ya Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.

Elimu kuwa Kipaumbele Kikuu

Ngombale Mwiru alisema moja ya vipaumbele vyake vikubwa ni kuboresha sekta ya elimu, akiamini kuwa taifa lolote lenye elimu bora hujenga msingi imara wa maendeleo.

Alieleza kuwa bado mazingira ya walimu ni duni, hivyo serikali yake itaboresha miundombinu ya shule, nyumba za walimu, pamoja na kuwaunganishia intaneti (Wi-Fi) bure.

“Nahitaji walimu wakae katika mazingira mazuri. Nitawapandishia mishahara yao na hata kuiongeza mara dufu. Ikiwa mwalimu analipwa laki tano, mimi nitamfanya alipwe hadi milioni moja,” alisema.

Afya na Miundombinu ya Barabara

Kuhusu sekta ya afya, alisema serikali yake itajenga zahanati katika kila eneo la nchi, na kujenga nyumba za madaktari karibu na vituo hivyo ili huduma zipatikane kwa haraka. Pia aliahidi kuboresha mishahara ya watumishi wa kada ya afya.

Vilevile, Ngombale Mwiru aliahidi kujenga barabara za zege katika maeneo yote yenye changarawe ili kuboresha usafiri na biashara za wananchi.

Kilimo na Ajira za Vijana

Akiwa mgombea kutoka Chama cha Wakulima, Ngombale Mwiru alisema serikali yake itakuwa ya kimapinduzi katika sekta ya kilimo kwa kutoa trekta moja kwa kila kaya kumi, hatua itakayosaidia kukuza kilimo cha kisasa na kuongeza uzalishaji.

Aidha, aliahidi kuwa serikali yake itawawezesha vijana kwa kuwapatia bodaboda kama njia ya kujiajiri.

“Nimegundua vijana wengi wanaendesha bodaboda. Nikichaguliwa, kila kijana asiye na ajira ataandikishwa na kupewa bodaboda ili aweze kujikwamua kiuchumi,” alisema.

Kupambana na Ufisadi

Ngombale Mwiru aliahidi kupambana vikali na vitendo vya ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma, akisema serikali yake haitavumilia viongozi wala watumishi watakaohusika.

Kwa utani wenye uzito, alisema ataanzisha bwawa maalum Ikulu lenye mamba wakali kwa ajili ya kuwaadhibu viongozi watakaothibitika kufanya ufisadi.

“Kutakuwa na siku maalum Ikulu ambapo mafisadi wataadhibiwa kwenye bwawa hilo la mamba nikiwa shuhuda,” alisema kwa msisitizo.


Mwisho

Comments