NI DAR CITY 'BAL QUALIFIERS' 2025 RC CHALAMILA AWAITA WANADARISALAMA KESHO
NI DAR CITY 'BALL QUALIFIERS'RC CHALAMILA AWAITA WANADARISALAMA KESHO
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewakaribisha wakazi wote wa jiji hilo kujitokeza kwa wingi kutazama mchezo wa kimataifa wa kikapu utakaofanyika kesho, tarehe 17 Oktoba 2025, katika viwanja vya Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) kuanzia saa moja jioni.
Amesema mchezo huo ni sehemu ya michuano ya kufuzu Ligi ya Afrika ya Kikapu (BAL Qualifiers), ukishirikisha timu kutoka Tanzania, Uganda na Komoro, ambapo mwenyeji wake ni timu ya Dar City Basketball.
“Hii ni fursa kwa wakazi wa Dar es Salaam kujionea michezo ya kiwango cha juu kabisa. Tunataka kuona viwanja vikiwa vimefurika mashabiki kuunga mkono vijana wetu,” amesema Chalamila.
Aidha, amewataka wazazi, vijana na wadau wa michezo kutumia fursa hiyo kuhamasisha ushiriki katika michezo kama njia ya kuimarisha afya na kujenga ajira kupitia vipaji.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma (Mwana FA), amesema mashindano hayo ni hatua muhimu kwa Tanzania kuonyesha uwezo wake katika mchezo wa kikapu, huku akiwapongeza Dar City Basketball kwa maandalizi bora na kujitoa kwao kuinua michezo nchini.
“Tunataka kuona Watanzania wanajitokeza kwa wingi kuishangilia Dar City. Huu ni wakati wetu kuonesha Afrika kuwa Tanzania inaweza,” amesema Mwinjuma.
Kapteni wa Dar City Basketball, Hashimu Thabiti, amesema timu yake ipo tayari kwa mchezo huo wa kesho na inawaomba mashabiki wajitokeze kuipa sapoti.
“Tumejipanga vizuri na tunataka ushindi. Mashabiki wetu watarajie burudani ya kipekee,” amesema Hashimu.
Naye Kocha wa Dar City, Pobi Gweye, amesema maandalizi yamekamilika kwa asilimia mia moja na wachezaji wako kwenye hali nzuri ya kushindana.
“Tunaiwakilisha Tanzania, na tutahakikisha tunafanya vizuri ili kuendelea kwenye hatua inayofuata ya Afrika,” amesema Gweye.
Mchezaji wa kimataifa kutoka Senegal, Souleymane Diabaté, amesema amehamasika sana kuona Tanzania ikiandaa mashindano ya kiwango cha juu kama hayo.
“Nimefurahishwa na jinsi Watanzania wanavyoupokea mchezo huu. Ni hatua kubwa kwa bara la Afrika,” amesema Diabaté.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuvutia mashabiki wengi wa kikapu jijini Dar es Salaam na kuleta hamasa mpya katika kukuza michezo nchini.



.jpeg)
Comments