NI DKT SAMIA TENA DAR, KUFANYA MIKUTANO YA KAMPENI SIKU TATU KUANZIA OKTOBA 21,RC CHALAMILA AWAITA WANANCHI
NI DKT SAMIA TENA DAR, KUFANYA MIKUTANO YA KAMPENI SIKU TATU KUANZIA OKTOBA 21,RC CHALAMILA AWAITA WANANCHI
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufanya mikutano ya kampeni jijini Dar es Salaam kwa muda wa siku tatu, kuanzia Oktoba 21 hadi Oktoba 23, 2025, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza kuhusu ujio wa mgombea huyo ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amesema Dkt. Samia atafanya mikutano katika viwanja vya Leaders Club (Kinondoni), viwanja vya TANESCO – Temeke, na viwanja vya Kinyerezi, ambapo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumsikiliza mgombea huyo akiwasilisha sera na mipango ya maendeleo kwa taifa.
RC Chalamila amewahakikishia wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhusu hali ya usalama, akibainisha kuwa mkoa huo utaendelea kuwa salama kipindi chote cha kampeni, wakati wa uchaguzi na hata baada ya uchaguzi. Amehimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchaguzi na kujitokeza kwa wingi kupiga kura ifikapo Oktoba 29, bila hofu wala vitisho.
Aidha, Chalamila amezungumzia changamoto ya upungufu wa maji jijini humo, akibainisha kuwa Serikali imechukua hatua madhubuti kutatua tatizo hilo kwa kudumu, ikiwemo kununua mashine mpya za kusukuma maji pamoja na utekelezaji wa mradi wa Bwawa la Kidunda, ambao utamaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Vilevile, RC Chalamila ameeleza kuwa upatikanaji wa umeme umeimarika, na Serikali inaendelea na juhudi za kukabiliana na changamoto za mafuriko kwa kujenga madaraja mapya katika maeneo ya Jangwani, Kigogo, Mkwajuni, Geti Jeusi na Nguva (Kigamboni).
Sambamba na hayo, Chalamila ameeleza kuwa Serikali imeboresha mfumo wa usafiri wa mwendokasi (DART), ambapo sasa inashirikiana na sekta binafsi kuboresha huduma hiyo. Amesisitiza kuwa daladala, bajaji na bodaboda hazitaruhusiwa kupita katika njia za mwendokasi ili kuhakikisha usafiri huo unabaki kuwa huduma ya haraka, salama na yenye ufanisi kama ilivyokusudiwa


.jpeg)
Comments