RC Chalamila Azindua Programu ya “Konekt Umeme, Pika kwa Umeme” — Mwanzo Mpya wa Mapinduzi ya Nishati Safi Tanzania

 

RC Chalamila Azindua Programu ya “Konekt Umeme, Pika kwa Umeme” — Mwanzo Mpya wa Mapinduzi ya Nishati Safi Tanzania







Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ameongoza uzinduzi rasmi wa programu ya “Konekt Umeme, Pika kwa Umeme” iliyobuniwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), hafla iliyofanyika leo katika viwanja vya Mwembe Yanga, wilayani Temeke.

Programu hiyo inakusudia kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi ya umeme kwa kupikia kwa gharama nafuu, ufanisi mkubwa, na urafiki kwa mazingira — ikiwa ni sehemu ya juhudi za kitaifa za kupunguza utegemezi wa kuni, mkaa, na gesi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Chalamila aliipongeza Wizara ya Nishati, TANESCO, na wadau wa maendeleo kwa ubunifu huo, akisema mpango huo ni hatua kubwa kuelekea mustakabali wa matumizi endelevu ya umeme nchini.

“Mpango huu ni mwanzo wa zama mpya katika historia ya huduma za umeme nchini, unaounga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza matumizi ya nishati safi,”
alisema Chalamila.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, mpango wa Konekt Umeme, Pika kwa Umeme unatekelezwa sambamba na dira ya kitaifa ya Energy Compact, ambayo inalenga kuwaunganishia umeme wateja milioni 8.5 ifikapo mwaka 2030 — sawa na wateja wapya milioni 1.7 kila mwaka.

Twange alibainisha kuwa kupitia programu hii, wateja wapya wa umeme watapatiwa jiko la umeme wakati wa kuunganishiwa huduma, na watakuwa na uwezo wa kulipia kidogo kidogo kupitia mfumo wa token, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa nishati safi majumbani.

Katika hatua ya kuhamasisha wananchi, RC Chalamila alikabidhi majiko ya umeme kwa baadhi ya wananchi na kuwataka kuwa mabalozi wa mabadiliko ya matumizi ya nishati safi katika jamii zao.

Comments