WANAFUNZI ZAIDI YA MILIONI 1.5 KUFANYA UPIMAJI WA KITAIFA WA DARASA LA NNE OKTOBA 22 NA 23, 2025

 WANAFUNZI ZAIDI YA MILIONI 1.5 KUFANYA UPIMAJI WA KITAIFA WA DARASA LA NNE OKTOBA 22 NA 23, 2025



Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam


Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza kuwa jumla ya wanafunzi 1,582,140 wa Darasa la Nne kutoka shule 20,517 nchini watafanya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne (SFNA) kuanzia tarehe 22 hadi 23 Oktoba, 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo,Prof Said Mohamed amesema kati ya wanafunzi hao, wavulana ni 764,290 sawa na asilimia 48.31, huku wasichana wakiwa 817,850 sawa na asilimia 51.69.

Prof Mohamed ameeleza kuwa kati ya wanafunzi wote walioandikishwa, asilimia 93.27 watafanya upimaji kwa Kiswahili, huku asilimia 6.73 wakifanya kwa Kiingereza, lugha ambayo wamekuwa wakitumia kujifunzia. Aidha, wanafunzi 5,750 wenye mahitaji maalum wamesajiliwa, wakiwemo wenye uoni hafifu, wasioona, wenye uziwi, ulemavu wa akili na ulemavu wa viungo.

Katibu Mtendaji huyo amesema kuwa mwaka huu upimaji huo utafanyika kwa mara ya kwanza kwa kuzingatia Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 (Toleo la 2023) na Mtaala ulioboreshwa.

Wanafunzi watafanya masomo sita ya msingi ambayo ni Sayansi, Hisabati, Jiografia na Mazingira: Sanaa na Michezo, Kiswahili, English Language, na Historia ya Tanzania na Maadili. Pia kutakuwa na masomo ya chaguo matatu — Kifaransa, Kiarabu, na Kichina — ambapo kila mwanafunzi atachagua somo moja tu.

Akifafanua umuhimu wa upimaji huo, Katibu Mtendaji alisema lengo ni kupima kiwango cha wanafunzi katika stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) pamoja na kubaini uelewa wao katika masomo wanayojifunza. Aliongeza kuwa matokeo ya upimaji yatasaidia walimu na wakuu wa shule kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.

Ameeleza kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika, ikiwemo usambazaji wa karatasi za upimaji na nyaraka zote muhimu katika Halmashauri zote nchini, sambamba na maandalizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji, Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri zimepewa jukumu la kuhakikisha vituo vyote vya upimaji vinakuwa salama na vinafuata miongozo ya NECTA.

Baraza pia limewataka wasimamizi wa mitihani kufanya kazi kwa uadilifu, umakini na weledi, kuhakikisha wanafunzi wote, wakiwemo wenye mahitaji maalum, wanapata haki zao. Wanafunzi wasioona watapewa mitihani ya nukta nundu, wenye uoni hafifu maandishi yaliyokuzwa, na wote wenye mahitaji maalum kuongezewa muda — dakika 20 kwa kila saa kwa somo la Hisabati na dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine.


Aidha, Baraza limewakumbusha wanafunzi kufuata kanuni za mitihani na kuepuka udanganyifu, likisisitiza kuwa mwanafunzi yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa kanuni.


Vilevile, wamiliki na wakuu wa shule wametakiwa kutojihusisha na usimamizi wa mitihani ndani ya vyumba vya mitihani, huku Baraza likionya kuwa litafuta kituo chochote kitakachohatarisha usalama wa upimaji huo.

Baraza pia limeiomba jamii kushirikiana kuhakikisha mazingira ya upimaji yanabaki salama na tulivu, na kwamba hakuna mtu asiyehusika atakayeingia katika maeneo ya shule wakati wa mitihani.

Katika hitimisho lake, Katibu Mtendaji ametoa wito kwa wadau wa elimu na wananchi wote kutoa ushirikiano wakati wa uendeshaji wa upimaji huo na kutoa taarifa za udanganyifu kwa mamlaka husika kupitia namba ya simu 0759 360 000 au barua pepe esnecta@necta.go.tz.

Baraza la Mitihani la Tanzania limewatakia wanafunzi wote kila la heri katika kufanya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne tarehe 22 na 23 Oktoba 2025.

Comments