Wengi Wamtaja Mgombea Urais wa CCM Kuongoza Uchaguzi wa 2025 — Utafiti wa CIP–Africa
Wengi Wamtaja Mgombea wa CCM Kuongoza Uchaguzi wa 2025 — Utafiti wa CIP–Africa
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Kituo cha Sera za Kimataifa Afrika (CIP–Africa) kimetoa matokeo ya utafiti wa kura ya maoni yanayoonyesha kuwa asilimia 84.5 ya Watanzania walioulizwa wanampendelea mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Akitangaza matokeo hayo leo Oktoba 22, 2025, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Tafiti na Uchapishaji wa CIP–Africa, Thabit Mlangi, alisema kuwa utafiti huo ulifanyika kati ya Septemba 30 hadi Oktoba 5, 2025, ukihusisha mikoa 19 — 17 ya Tanzania Bara na miwili kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
“Utafiti huu ulilenga kupata taswira ya hisia za wananchi kuhusu uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani,” alisema Mlangi.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, asilimia 3 ya washiriki walisema watampigia kura mgombea wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), asilimia 3 mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), asilimia 1.5 mgombea wa NCCR–Mageuzi, huku asilimia 8 wakisema kura yao ni siri.
Washiriki wa Utafiti
Jumla ya watu 1,976 walishiriki katika kura hiyo ya maoni — wanaume 988 na wanawake 988.
Kati yao:
-
29% walikuwa na umri wa miaka 18–25
-
32% walikuwa na miaka 26–35
-
13% miaka 36–45
-
17% miaka 46–55
-
9% walikuwa na zaidi ya miaka 55
Kwa upande wa elimu:
-
14% walikuwa na elimu ya msingi
-
57% elimu ya sekondari
-
28% elimu ya chuo
-
1% walikuwa na elimu nyingine
Mikoa iliyoshiriki ni pamoja na Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Iringa, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Ruvuma, Tabora, Tanga, na Kaskazini Pemba pamoja na Kaskazini Unguja.
Mwelekeo wa Kisiasa na Ushiriki wa Kampeni
Mlangi alisema kuwa asilimia 81 ya washiriki wanajiona kama wafuasi au wafuatiliaji wa masuala ya siasa, huku 19% wakisema hawana ufuatiliaji wa karibu wa kisiasa.
Kati ya wanaofuatilia siasa, 57% ni wanaume na 43% ni wanawake.
Aidha, asilimia 53 ya waliohojiwa walihudhuria mikutano ya kampeni za vyama vya siasa.
Kati yao:
-
76% walihudhuria mikutano ya CCM
-
15% ya ACT–Wazalendo
-
2% ya CHAUMMA
-
7% walihudhuria mikutano ya vyama zaidi ya kimoja
Sera, Vipaumbele na Ushiriki wa Uchaguzi
Kwa upande wa ushawishi wa sera, asilimia 46 ya washiriki walisema wameshawishiwa na sera za vyama vya siasa, huku 54% wakisema hawajashawishiwa.
Kuhusu ushiriki wa uchaguzi, asilimia 83 wamethibitisha kuwa watapiga kura Oktoba 29, 2025.
Washiriki walitaja vipaumbele wanavyotaka rais ajaye avipe kipaumbele kuwa:
-
Maji safi na salama (78%)
-
Elimu bora (78%)
-
Miundombinu ya barabara na madaraja (69%)
-
Huduma bora za afya (63%)
-
Mapambano dhidi ya rushwa (60%)
-
Uimarishaji wa demokrasia (47%)
Baadhi ya wananchi, hasa wa Ilala na Segerea, walionyesha hofu kuhusu kuongezeka kwa matumizi ya dawa za kulevya aina ya bangi miongoni mwa wanafunzi, wakimtaka rais ajaye kulipa kipaumbele suala hilo.
Maandalizi ya Uchaguzi
Mlangi aliongeza kuwa asilimia 91 ya washiriki wameridhishwa na utendaji wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), wakieleza kuwa tume imeonyesha uwazi na umakini katika maandalizi ya uchaguzi.
Hata hivyo, alisema kuwa matokeo ya kura ya maoni kwa Wabunge na Madiwani bado yanachambuliwa kutokana na mkanganyiko wa taarifa, na ripoti kamili inatarajiwa kutolewa wiki ijayo.


.jpeg)
Comments