KAULI YA RUWA'ICHI YAWAIBUA VIJANA WENGINE KATOLIKI WADAI KUWAPEPEKA VATIKANI YEYE NA KITIMA
KAULI YA RUWA'ICHI YAWAIBUA VIJANA WENGINE KATOLIKI WADAI KUWAPEPEKA VATIKANI YEYE NA KITIMA
Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam
Upinzani mkali na usio na kificho umeibuka ndani ya Kanisa Katoliki baada ya waumini, Mackdeo Shilinde na Gerald Abel, kupinga hadharani kauli walizodai kutolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, wakisema mimbari imegeuzwa jukwaa la matusi, hukumu na vitisho badala ya Injili ya mapendo na umoja.
Katika tamko lao, waumini hao wamesema hawatakubali Kanisa liendeshwe kwa woga na matusi, wakisisitiza kuwa Kanisa si mali ya Askofu wala Padri mmoja, bali ni jumuiya ya waumini.
Kwa mujibu wa waumini hao, Askofu Ruwa’ichi alitumia homilia ya Misa ya Krismasi tarehe 25 Desemba 2025 kuwaita waumini kwa maneno mazito kama “lofa”, “mpumbavu”, “njaa njaa”, “msaliti” na “ndumilakuwili” — kauli walizosema zinakiuka moja kwa moja mafundisho ya Biblia.
Waumini hao wamenukuu wazi Maandiko Matakatifu yanayokataza hukumu na udhalilishaji, wakisema:
*“Msihukumu, msije mkahukumiwa.” (Mathayo 7:1)*
*“Usimhukumu mtumishi wa mtu mwingine.” (Warumi 14:4)*
*“Neno lenu na liwe daima na neema.” (Wakolosai 4:6)*
Kwa mujibu wa waumini, hakuna sehemu ya Biblia inayoruhusu kiongozi wa dini kuwaita waumini wake majina ya kudhalilisha hadharani, hasa kutoka madhabauni.
Katika msimamo wao, waumini hao wamesisitiza kuwa mimbari imewekwa kwa ajili ya kuunganisha waumini na kuwafariji, si kuwadhalilisha. Wamenukuu pia:
*“Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu.” (Mathayo 5:9)*
*“Jitahidini kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.” (Waefeso 4:3)*
Wamesema kauli za matusi kutoka madhabauni zinawakwaza waumini, kinyume na onyo la Biblia linalosema:
*“Msiwakwaze wadogo hawa.” (Mathayo 18:6)*
Shilinde na Abel wamesema kauli hizo hazikujibu hata hoja moja kati ya zile zilizowasilishwa kwa mamlaka za juu za Kanisa kupitia barua ya waumini Stanslaus Nyakunga na Elia Phaustine kwa Balozi wa Vatican.
Barua hiyo iliomba tathmini ya mwenendo wa Padri Charles Kitima, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), anayelalamikiwa kuhusishwa na siasa.
Kwa mujibu wa waumini, badala ya hoja kujibiwa kwa busara au kufanyiwa uchunguzi wa kikanisa, walishuhudia waumini wakiburuzwa hadharani kwa maneno ya dharau.
Waumini hao wamesema kwa msimamo mkali kwamba Kanisa Katoliki halipaswi kuingizwa katika siasa za chama chochote, wakisisitiza kuwa Padri au Askofu anapaswa kuwa muunganishi wa waumini na Taifa, si mshauri wa chama cha siasa.
“Padri si Kanisa, Askofu si Kanisa — Kanisa ni waumini,” wamesisitiza, wakiongeza kuwa Kanisa linapaswa kuwa kimbilio la wote, si kumbatio la wachache wenye sauti au mamlaka.
Katika hatua inayozidisha mvutano huo, Shilinde na Abel wametangaza kuwa watapeleka malalamiko rasmi kwa Balozi wa Vatican nchini Tanzania, wakidai:
• Padri Charles Kitima achunguzwe kwa kuingiza Kanisa katika siasa za chama kimoja na kuchafua taswira ya Kanisa Katoliki;
• Askofu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi achukuliwe hatua za kikanisa kwa kuwatukana waumini hadharani na kuwavua hadhi ya Ukristo kwa kauli za mimbari.
Wamesema hatua hiyo inalenga kulilinda Kanisa dhidi ya matumizi mabaya ya mimbari na dhidi ya kuligeuza Kanisa kuwa jukwaa la mapambano ya kisiasa.
Hatua hiyo imezidisha mjadala mzito ndani ya Kanisa Katoliki kuhusu mipaka ya mamlaka ya uongozi wa dini, haki ya waumini kuhoji, na wajibu wa viongozi wa kiroho kuheshimu Injili wanayoihubiri.
Kwa sasa, macho ya waumini, wachambuzi wa masuala ya dini na wadau wa Kanisa yameelekezwa Vatican, ambako inasubiriwa iwapo kutachukuliwa hatua za kikanisa kufuatia malalamiko hayo mazito.



Comments